WAKATAOVUJISHA SIRI ZA TAKWIMU KUTUPWA JELA


WADADISI watakaovujisha siri za takwimu watakazokusanya za mapato na matumizi ya kaya binafsi, watashtakiwa mahakamani kwani watakuwa wametenda kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametoa msimamo huo wakati wa Kufunga Mafunzo ya Wadadisi na Kuzindua Ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania mwaka 2017/2018 mjini Dodoma jana.

“Mnaenda kukusanya takwimu, taarifa hizi ni za siri, hamtakiwi kuzitoa popote kwa kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kitakwimu tu. Mkifanya vinginevyo, ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya mwaka 2015,” alisema Waziri Mpango.

Aliwatahadharisha wadadisi hao 620 kuwa wamepewa dhamana ya kukusanya takwimu katika nchi nzima, hivyo ni lazima wazingatie masharti ya sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Dk Mpango aliwaagiza viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri, tarafa, kata hadi vijiji, kuwapa ushirikiano wadadisi hao wakati wanapofika kukusanya takwimu za mapato na matumizi ya kaya binafsi katika maeneo yao.

Aidha, aliwataka wananchi wote nchini ambao kaya zao zimechaguliwa kushiriki katika utafiti huo, kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi za kila mwanakaya wa kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea.

Dk Mpango aliwataka vijana hao wanaokwenda kufanya utafiti na kukusanya takwimu za kaya binafsi 10,460 katika Tanzania Bara kuanzia Novemba mwaka huu hadi Novemba 2018, watambue kwamba wamepewa ajira, hivyo waitumie fursa hiyo vizuri kwa kukusanya takwimu sahihi bila kuzipika.

Alisema wizara yake inahitaji takwimu hizo za hali ya umasikini mapema iwezekanavyo ili kuzitumia wakati wa bajeti mwakani, lazima serikali ipate matokeo ya awali ya hali ya umasikini hapa nchini ili kuzitumia takwimu za miezi sita ya mwanzo.

Dk Mpango alisema, utafiti huo utaiwezesha serikali kupima kiwango cha hali ya umasikini wa kipato, chakula na pengo baina ya matajiri na masikini kuanzia kipindi cha mwaka 2013 hadi sasa.

“Kukamilika kwa utafiti huu kutaiwezesha serikali kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo ya kitaifa yaliyoanishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) na malengo ya Maendeleo Endelevu 2030,” alisema.

Alisema utafiti kama huo uliowahi kufanyika kabla, umeonesha kwamba kiwango cha umasikini wa kipato kinaendelea kupungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 28.2 mwaka 2011/12.

Waziri Mpango alisema pamoja na mafanikio hayo, changamoto za maendeleo bado zipo na ndiyo maana serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine inaendelea na juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za msingi za kijamii kadiri uchumi unavyokua na hivyo kupunguza kama si kumaliza kabisa na umasikini,” alisema.

Alisema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyo chini ya Mkurugenzi Mkuu, Dk Albina Chuwa inaendelea na kazi ya kusimamia na kuhakikisha ubora wa kazi hiyo kwa kutumia njia za kisasa ambazo zitaiwezesha kupata taarifa za uendeshaji za kila siku za kila mdadisi.

Akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Chuwa aliwataka wadadisi hao kwenda kufanya kazi ya kukusanya takwimu za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya masikini kwa weledi na kwa umakini mkubwa na kuhakikisha katika kipindi cha miezi sita ya mwazo wanatoa matokeo ya awali.

Aidha Dk Chuwa alisema utafiti huo utakaogharimu Sh bilioni 10 hadi kukamilika, ni nusu ya fedha zilizotumika katika utafiti kama huo uliotangulia ambao ulitumia Sh bilioni 20, utafiti huo una gharama ndogo kutokana na kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa katika kukusanya takwimu hizo.

Akitoa neno la shukrani, Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya Tehama Ofisi ya Rais-Tamisemi, Baltazar Kibola alisema wizara yake itahakikisha inawapa ushirikiano wadadisi hao kwa kutumia wataalamu wa Tehema waliopo katika mikoa mbalimbali nchini “Wadadisi vifaa vyenu vitakapokuwa vimeleta hitilafu basi tumieni wataalamu wa Tehama waliopo katika halmashauri mbalimbali kuvitengeneza ili utafiti wenu usikwame,” alisema

IMEANDIKWA NA MAGNUS MAHENGE, DODOMA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post