Afisa Tarafa ya Chala, Diana Khan
**
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya Chala iliyopo katika Kata ya Chala wilayani Nkasi mkoani Rukwa, wamepiga kura za siri ambayo walimu watatu wa kiume wamepigiwa kura nyingi wakituhumiwa kuna mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Kutokana na matokeo hayo ya kura za siri, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda amemuagiza Ofisa Elimu Wilaya ya Nkasi (Sekondari), Abel Ntupwa kuwasimamisha kazi walimu hao watatu ili kupisha uchunguzi Pia amemwagiza amvue madaraka Mratibu Elimu Kata ya Chala, kwa kushindwa kusimamia shule zake hadi walimu wanajihusisha na vitendo vya kuwatongoza wanafunzi.
Upigaji kura huo uliwahusisha wanafunzi wa Kidato cha Tatu na cha Pili, na kushuhudiwa na viongozi watendaji wa kata hiyo wakiongozwa na diwani Michael Mwanalinze na walimu wote wa shule hiyo.
Ulifanyika jana shuleni Chala na kusimamiwa na mkuu wa wilaya, na kura zilikuwa za siri, lengo likiwa ni kuwatambua walimu wa kiume wenye mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike shuleni hapo.
“Katika zoezi hili walimu watatu wameibuka kidedea kwa kupigiwa kura nyingi za siri... bado ni siri majina yao sitayataja hadharani kwa sasa isipokuwa ninaondoka nayo...,” alisema Diwani Mwanalinze, akizungumza kwa uchungu, alisema ni kweli walimu wanafanya mapenzi na wanafunzi na kuwa hatua aliyoichukua mkuu wa wilaya ni nzuri.
Ofisa Elimu Sekondari, Ntupwa alisema atalifanyia kazi agizo la DC la kumvua madaraka Mratibu wa Elimu Kata. Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa wilaya ya Nkasi inaongoza kimkoa kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatiza masomo kutokana na ujauzito, kwani kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, wanafunzi 155 wamekatiza masomo kutokana na kupata ujauzito.
IMEANDIKWA NA PETY SIYAME - HABARILEO NKASI