NAIBU Waziri wa nchi Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , George Joseph Kakunda ameuagiza uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi kuwachukulia hatua kali ya kinidhamu na kijinai mara moja ikiwemo kuwafukuza kazi walimu wanaofanya mapenzi na wanafunzi wao wa kike .
Naibu Waziri alielezwa kuwa walimu hao wamekuwa wakidai kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao ni sehemu ya ruzuku yao ya ualimu
Kufuatia tabia hizo za walimu hao Kakunda alitoa agizo hilo kwa viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Mpanda alipokuwa akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Nsimbo akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika mkoa wa Katavi .
Awali kabla agizo hilo halijatolewa , Diwani wa kata ya Katumba , Seneta Baraka alimweleza Naibu Waziri Kakunda kuwa maisha yake yako hatarini kutokana na kuwafuatilia kwa karibu walimu walio na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike .
Aliongeza kuwa baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule mbili za sekondari za Katumba na Kenswa zilizopo katika makazi ya wakimbizi ya Katumba wamekubuhu katika kufanya mapenzi na wanafunzi wao wa kike huku wengine wakiwa wamewaoa wanafunzi wao wakiwa bado hawajamaliza masomo yao .
“Baadhi ya walimu wanadai kuwa kufanya mapenzi na wanafunzi wao ni sehemu ya ruzuku yao ya ualimu ….. nimekuwa nikipata ushirikiano hafifu na uongozi wa wilaya licha ya kutoa taarifa kwao zinazohusu tabia hizo za walimu hao
Hata hivyo uongozi wa wilaya umeshindwa kuwachukulia walimu hao hatua za kinidhamu na kijinai licha ya kuwepo ushahidi wa kutosha …. Badala yake nimekuwa nikitishiwa maisha “ alisema.
Alimweleza Naibu waziri kuwa yupo mwalimu mmoja anayefundisha kati ta shule hizo mbili za sekondari ambaye ameamua kumuoa mwanafunzi wake wa kike ambaye amelazimika kukatiza masomo yake .
“Nilishatoa taarifa ya mwalimu huyu na wengine wenye mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike katika vikao vya baraza la madiwani lakini hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa dhidi yake baada yake baadhi ya madiwani wenzangu wamevujisha siri za vikao na kwenda kuwataarifu walimu hao kuwa mimi ndiyo ninaye washtakia” alieleza .
Alieleza kuwa mwalimu huyo baada ya penzi na mwanafunzi wake wa kike kukolea aliamua kuishi kinyumba na mwanafunzi huyo hadi sasa ambapo tayari ameshalipa mahari kwa wazazi wa msichana huyo.
Alisema kuwa hata hivyo mama mzazi wa msichana huyo amekataa katakata kupokea posa ya mwalimu huyo .
Alimuomba Naibu Waziri amsaidie ili aweze kupatiwa ulinzi wa kutosha kwa kuwa maisha yake yako hatarini kutokana na vitisho anayopewa kwamba hata siku hizi amelazimika kupunguza kutembelea maeneo ya starehe akihofia maisha yake .
Mara baada ya kupokea maelezo hayo Naibu Waziri Kakunda aliungiza uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Mpanda kuhakikisha inawachukulia hatua kari ikiwemo kuwafukuza kazi walimu wote watakao bainika kufanya mapenzi na wanafunzi kwa kisingizio kuwa ndio ruzuku yao walimu kufanya mapenzi na walimu.
Alisema sheria inakaza mtu kufanya mapenzi na mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 hivyo wanaofanya hivyo watambue kuwa wanafanya makosa na wala hakuna mtu kusingizia kuwa wlikubaliana .
Kakunda alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha mtoto anasoma kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne hivyo aliwaonya wanaowaozesha wanafunzi wakae chonjo kwani kufanya hivyo ni kosa kubwa .
Alizitaka kamati za ulinzi na usalama za Kata hapa nchini zishirikiane kufanya kazi ya kuhakikisha zinadhibiti mimba za wanafunzi kwenye kata zao .
Afisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri ya Nsimbo Said Malamba alisema baadhi ya walimu wanaotuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi wao tayari wameisha anza kulishughulikia.
Alisema na tayari walimu wawili wawili wa shule ya Sekondari Katumba na mmoja wa Seokndari ya Kenswa walishaandikiwa barua na tume ya utumishi ya kujieleza kutokana na tuhuma hizo na baada ya kujieleza tayari Mwalimu Mmoja wa Shule ya Msingi Katumba Mwalimu Fransis Manyala amechukuliwa hatua na walimu wawili hawakupatikana na hatia.
Alisema mwalimu huyo aliyepatikana na hatia kwenye tume ya utumishi ya Wilaya ya Mpanda amekata rufaa kwenye tume ya utumishi ya Taifa baada ya kutoridhika na maamuzi ya kusimamishwa kwake kazi .
Na Walter Mguluchuma- Malunde1 blog Katavi
Social Plugin