22 CCM WACHUANA UPYA KURA ZA MAONI JIMBO LA NYALANDU


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewaonya viongozi wa chama hicho ambao amesema wanawagawa wananchi.

Amesema endapo wataendelea kufanya hivyo watavuliwa uongozi.

Kinana amesema hayo leo Alhamisi Desemba 14,2017 akifungua mkutano wa halmashauri kuu ya jimbo unaopiga kura ya maoni kupata mgombea ubunge jimbo la Singida Kaskazini.

Katika kinyang’anyiro hicho cha marudio wagombea 22 wamejitokeza kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Lazaro Nyalandu aliyejivua ubunge alioupa akiwa CCM na sasa amejiunga Chadema.

Amesema CCM ipo imara na wapambe wamepungua kwa kiasi kikubwa. Amewataka wagombea wafanye kampeni zinazofaa na mmoja akichaguliwa, wote wawe wamoja ili chama hicho kishinde kwa kishindo.

Kinana akizungumza katika mkutano huo unaofanyika Kijiji cha Ilongero, Singida amesema uchaguzi wa awali uligubikwa na vitendo vya rushwa ndipo uongozi wa juu wa CCM ulipoamua kufuta mchakato.

Ameagiza vitendo hivyo visijirudie akiwataka wajumbe wasirubuniwe kwa aina yoyote; na wagombea wakatae maombi ya wapiga kura ambao mara nyingi huwaambia unatuachaje.

Kinana amempongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Hassan Kilimba akisema amekuwa mwaminifu kwa chama hicho hata baada ya kuacha ubunge.

Na Gasper Andrew, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post