FAMILIA ya mwanamuziki wa dansi, Nguza Viking ‘Babu Seya’ aliyepewa msamaha na Rais John Magufuli imepata pigo, kutokana na kifo cha mdogo wa mwanamuziki huyo, Chimbuza Chrizoo kilichotokea saa chache baada ya kuachiwa kwao huko.
Babu Seya akiwa na mwanawe, Papii Kocha walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, baada ya kukutwa na hatia kwenye kesi ya kulawiti. Walitumikia miaka zaidi ya miaka 13.
Wiki iliyopita katika sherehe za Uhuru, Rais John Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa wa kifungo cha kawaida na maisha, ambapo wawili hao nao walipata msamaha huo.
Siku hiyo hiyo majira ya saa 12 walitolewa kwenye Gereza la Ukonga na kupokewa kwa shangwe na Wakongo waishio nchini na wale wa nchini Kongo, akiwamo huyo Chrizoo, ambae alikufa baada ya kusherehekea kuachiwa kwa ndugu zake hao.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia hiyo, mwanamuziki mkongwe nchini, Kikumbi Mwanza Mpango maarufu King Kiki, Chrizoo alikufa akiwa usingizini baada ya kumalizika kwa sherehe za kupongeza kuachiwa huru kwa Nguza.
King Kiki alisema baada ya kutolewa kwa msamaha watu mbalimbali nchini Congo walishangilia na kufikia hatua ya kuandaa sherehe, ambapo walikunywa na kucheza wakisherehekea msamaha huo.
Alisema, wakiwa walisherehekea hadi saa nane usiku huku wakinywa na kufurahia msamaha huo wa Rais Magufuli kwa wanamuziki hao.
Alisema, sherehe hiyo ilifanyika nyumbani kwa Chrizoo mkoa wa Katanga jijini Lubumbashi.
Alisema walisitisha sherehe hizo saa 8 usiku na Chrizoo aliingia ndani kulala.
Alipoingia kulala, hakuamka tena kesho yake, kwa kuwa alifia usingizini. Ndugu zake walipokuja kumwamsha kesho yake mchana, walishangaa kuona haamki.
Alisema, kwa sasa wameshamzika ndugu huyo nchini DRC na kuwa mwanamuziki Nguza na familia nzima imepokea kwa uchungu taarifa hiyo ya kifo.
“Ni jambo pia la kumshukuru Mungu kwa kuwa ndiye anayepanga, kwa sasa familia hii licha ya kufurahia kutolewa kwa ndugu yetu lakini pia tumepoteza tena ndugu mwingine, familia ya Nguza kule Congo ilisikia habari ya kuachiwa kwa ndugu yetu huyu kwenye vyombo vya habari na hapo hapo ilianza furaha,” alisema King Kiki.
Akizungumzia kwa nini mwanamuziki Nguza hasikiki akizungumza kwenye vyombo vya habari, alisema kuwa ataendelea kutosikika hadi baada ya wiki mbili ziishe. Alisema kwa sasa anaendelea na shughuli zake za kawaida akiwa amefichwa mahala, ambapo anakuwa yupo yeye Nguza na mwanawe Papii Kocha hadi ziishe wiki hizi mbili.
Akizungumzia sababu ya kufanya hivyo, King Kiki alisema kuwa ni utaratibu wa familia ambao imeuweka kwa wanamuziki hao kuwa kimya kwa muda huo, lakini ukimya huo pia sio wa bure, ila wanaandaa kitu kikubwa.
“Kwa sasa waandishi hamtomuona kwanza hadi zipite wiki hizo mbili ;na zikiisha tu Nguza na Papii mtawasikia na kuwahoji kila kitu. Hapo sasa watakuja vipi na wataeleza kitu gani wanakifanya ndani ya wiki hizo mbili,” alisema King Kiki.
Aliongeza, “Hata hivyo ifahamike kuwa familia inamshukuru sana tena sana Rais wetu John Magufuli, familia na Wakongo wote tulishtushwa na kuachwa bumbuwazi baada ya msamaha huo wa Magufuli. Mungu amzidishie mengi zaidi.”
Gazeti la Habarile liliwasiliana na mtoto wa kwanza wa Babu Seya, aitwae Monica ambaye kwa upande wake aliweka wazi kuwa familia imekuwa ikienda mara moja moja kuwaona akina Nguza na Papii Kocha; na kuongeza kuwa wamekubaliana wawaache kwanza wapumzike.
Bila ya kubainisha jina la hoteli, alisema kuwa ipo Mbezi Beach. Monica alisema watoto, wajukuu na vitukuu, wamekuwa wakienda kuwaona, lakini pia sio mara kwa mara ili kuwapatia muda wa kupumzika.
Aliongeza kuwa Papii Kocha hutumia muda kufanya mazoezi na kucheza mpira, huku Nguza hutumia muda wake mwingi kukaa zaidi akijiliwaza. Alieleza kuwa familia inaendelea kumshukuru na kumwombea baraka Rais Magufuli.
Akizungumzia ilivyopokea habari ya kuachiliwa kwa Nguza na mwanawe, alisema kwa upande wa familia hapa Dar es Salaam kila mtu alipokea kwa furaha. Alisema yeye alikuwa mkoani Morogoro na alitoka akiendesha gari kwa spidi kuwahi Gereza la Ukonga kuwaona Nguza na Papii wakitoka.
Tangu kutolewa, wawili hao wamekuwa wakitamba na nyimbo zao kama Seya na Salima. Nyimbo zao hizo zimekuwa zikichezwa zaidi kwenye redio.
Mashabiki wa muziki wamekuwa na shauku ya kusikia kama mzee Nguza ataendelea na muziki au atakuwa mlokole, kama alivyokuwa akisema wakati akiwa gerezani. Mapromota nao wamekuwa wakihangaikia dili la kuandaa onesho la kwanza la wawili hao, iwapo wataendelea kuimba
Chanzo- Habarileo