Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKOFU AHOJI MIPAKA YA SIASA NA DINI...ATAKA WANANCHI KUTOJENGEWA HOFU YA KUTOA MAONI


 Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza amehoji mipaka ya kuzungumzia masuala ya siasa na dini, huku akitaka wananchi kutojengewa hofu ya kutoa maoni yao.


Kauli ya askofu huyo inafanana na iliyotolewa na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo katika ibada ya Krismasi Jumatatu iliyopita kwamba kuna baadhi ya watu wanawajengea wananchi hofu ili wasiweze kutumia uhuru wao kutoa mawazo.


Askofu Bagonza alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mwandishi wetu, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuweka ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook, akihoji sababu za watu kuwasakama viongozi wa dini wanaojadili masuala ya siasa.


Alipotakiwa kuthibitisha kama ujumbe huo ni wa wake, Askofu Bagonza alisema “Ni kweli ni wa kwangu na kama huuoni, vijana watakuwa wamechezea mtandao.”


Ujumbe huo unasema, “Wakijenga shule hawaingilii wizara ya elimu, wakijenga hospitali hawaingilii wizara ya afya, wakijenga kisima cha maji hawaingilii wizara ya maji. Wakiombea mvua hawaingilii mamlaka ya hali ya hewa.


“Wakihimiza kilimo hawaingilii wizara ya kilimo, wakitoa msaada wa dawa kwa mgonjwa, wanapongezwa, wakihoji kwa nini hakuna dawa hospitali, wanaambiwa wanachanganya dini na siasa na wakikosoa mfumo wa kisiasa, wanaambiwa wanaingilia siasa! Kuna kitu hakiendi sawa.”


Akifafanua kuhusu ujumbe huo alisema, “Tujenge utamaduni wa kujenga hoja na kutotukanana matusi. Kuna watu wengine wanaamini uhuru wa kusema umetoweka. Nasema, kuwapa uhuru watu kusema na kutoa mawazo yao kunajenga kuliko kuwazuia au kuwajengea hofu.”


Askofu Bagonza pia alizungumzia madai kwamba viongozi wa dini wamekuwa wakimya sasa, “Si kama huko nyuma tulikuwa tunasema na sasa hatusemi hapana, Krismasi hii tumeanza kusema, lakini tukisema mnasema tunasema sana, tukikaa kimya mnasema tunakaa kimya.”


Alisema haki huliinua Taifa na mlinzi mkubwa wa amani ni haki.


“Vyombo vya dola wanahitaji haki, kila mtu anahitaji haki na silaha pekee ya amani ni haki. Tuwape uhuru watu waseme bila kuwazuia, tujenge utamaduni wa kujenga hoja,” alisema.


Askofu Shoo akihubiri katika ibada Krismasi kwenye Usharika wa Moshi Mjini wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo alisema watu wanajazwa hofu ili wasiseme ukweli wa kile wanachokiamini.


“Kuna watu wanajaribu kuwajaza watu hofu ili watu wasiseme ukweli na wasikae katika kweli. Watu wanajazwa hofu ili wasitetee kile wanachokiona ni cha haki,” alisema Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa dayosisi hiyo.


Alisema, “Watu wanajazwa hofu ili wasiwe huru kutoa mawazo wanayojisikia kuhusu Kristo, nchi yao na imani yao. Tukidumu katika kweli inatupa nguvu na uhuru wa kusema na kutembea bila woga.”


“Yesu amezaliwa si kutuletea tu neema lakini anatuletea kweli kuhusu maisha ya hapa duniani. Mafundisho yanatufundisha tumpokee ili atawale maisha yetu. Tudumu katika ukweli huu na daima tusimame katika kweli hiyo, wala tusione aibu wala tusione woga wa kusimama katika kweli hiyo. Wala tusione woga wa kutetea kweli hiyo,” alisema.

Na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com