Baada ya Rais John Magufuli kutangaza msamaha kwa zaidi ya wafungwa 8,000 juzi kwenye maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika, wananchi wengi walifurahi bila kufahamu changamoto watakaokutana nazo walioachiwa.
Kilichowafurahisha wengi ni kuachiwa huru kwa mamilia ya mwanamuziki maarufu, Nguza Viking pamoja na mwanaye, Johnson Nguza. Mwanamuziki huyo anayefahamika zaidi kama Babu Seya na Nguza maarufu kama Papii Kocha, waliachiwa jana.
Vyombo vya habari na mamia ya wananchi walijitokeza kuwalaki wafungwa hao walipokuwa wakiungana na familia yao, ndugu jamaa na marafiki.
Babu Seya na mwanaye ni pekee kwenye orodha ya waliopata msamaha wa Rais kati ya wafungwa 666 waliohukumiwa kifungo cha maisha.
Wamo pia 61 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa. Hao ni miongoni mwa 522 wanaosubiri kutekelezwa kwa adhabu hiyo.
Kwa jumla, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 8,157 wakiwamo 1,828 walioachiwa huru na 6,329 waliopunguziwa adhabu. Jana, taarifa ya ikulu ilisema Rais Magufuli amesha saini nyaraka za msamaha huo.
Msamaha wa Rais unapunguza msongamano uliopo kwenye magereza yote nchini ambao kabla ya uamuzi wake, Rais alisema kulikuwa na jumla ya wafungwa 39,000.
Taarifa za Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Magereza (WPB) mwaka 2015, zinaonyesha kulikuwa na wafungwa 31,382 ambao ni sawa na asilimia 115.7 ya uwezo wa magereza yote nchini kuhifadhi wafungwa.
Kwa wakati huo, WPB ilisema uwezo wa Tanzania ni kuhifadhi wafungwa 29,552. Hata hivyo, juhudi kubwa zinafanywa kuboresha mazingira ya watuhumiwa na wafungwa waliopo magerezani.
Miongoni mwa njia zinazotumika kutekeleza hilo ni mpango wa parole unaowaandaa wafungwa wanaoonyesha utiifu kupewa msamaha wa Rais anayepewa mamlaka hayo na Ibara ya 45(1) ya Katiba ya nchi.
Wanarudije uraiani?
Ni wawili tu kati ya wafungwa 1,800 walioachiwa huru jana taarifa zao zinafahamika. Babu Seya na mwanae. Ni kutokana na kupokea na vyombo vya habari walikoonekana wamebadilika na kurudi kwenye jamii waliyopotezana nayo kwa zaidi ya miaka 10 ya kukaa gerezani.
Ratiba ya familia ya Babu Seya imejaa kwa wiki hii. Mapromota wa muziki wa dansi na kila mdau anayefahamu umuhimu wa wanamuziki hawa, anatamani kufanya nao kazi.
Kwa picha zilizosambazwa juzi na jana baada ya kuachiwa kwao, walionekana wamebadilika. Walikuwa nadhifu wanaoweza kualikwa popote. Walipokelewa na watu maarufu wenzao na kukaribishwa uraiani.
Wakati anatangaza msamaha wake, Rais Magufuli alisema kuna watu wametumikia kifungo kwa muda mrefu akimtolea mfano mtu aliyefungwa akiwa na miaka 18 na sasa hivi ana zaidi ya miaka sitini.
“Yupo mzee mmoja, anaitwa Mganga Matonya, ana miaka 85 na ameshakaa gerezani miaka 37 baada ya kuhukumiwa ukiacha saba ya kusubiri hukumu. Jumla amekaa miaka 44,” alisema Rais.
Baada ya miaka 44 mzee Matonya anarudi uraiani. Ndani ya muda huo aliokuwapo jela, wamezaliwa Watanzania kadhaa waliokuwa na ushawishi kwenye maeneo tofauti.
Wafungwa wa mfano wa mzee Matonya ni wengi ambao wakirudi mtaani wanaweza wasikumbuke chochote. Mitaa imebadilika. Vijana wenzao waliokua na kucheza nao huenda mola alishawachukua. Hawatawakuta viongozi wa Serikali za Mitaa waliowaacha.
Mkuu wa magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Augustine Mboje anasema wafungwa wanaostahili msamaha hutoka kama walivyoingia na kurudishwa walipokuwa wanaishi.
“Kama wametoka mbali, husafirishwa mpaka kijijini kwao. Waliopo mjini, huwasiliana na ndugu zao. Hakuna wanachopewa kwa ajili ya kwenda kuanzia maisha mapya,” alisema kamishna huyo.
Kwa wanaoachiwa bila kuwa na uhakika wa waendako hali yao ni mbaya zaidi. Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema endapo tathmini ya kina haitofanywa, msamaha huu unaweza kuharakisha kifo chao.
“Yupo kijana mmoja ambaye baada ya kukaa gerezani kwa miaka 17 alishinda rufaa yake na akaachiwa. Aliporudi uraiani akakuta mambo mengi yamebadilika. Ndugu zake wamehama na hana pa kwenda. Alikuja ofisini kwetu na kutuambia taka hapo akisubiri kifo chake,” alisema Dk Bisimba.
Suluhisho
Kutokana na baadhi yao kushindwa kumudu mmaisha ya uraiani baada ya kutumikia vifungo vyao, Kamishna Mboje anasema Jeshi la Magereza limependekeza uandaliwe utaratibu utakaowawezesha wafungwa kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato.
“Watakaokuwa wanashiriki shughuli hizo watatunziwa fedha zao ambazo zitawasaidia wakitoka. Baadhi ya mataifa yamefanikiwa kwenye hili. Serikali ikiridhia, sisi pia tutakuwa na utaratibu huo,” alisema.
Alisema. Zamani, kuna baadhi ya wafungwa walikuwa wanakataa kutoka gerezani hata baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao au kupewa msamaha wa Rais.
Licha ya kutunziwa fedha kama jeshi hilo linavyopendekeza, Dk Bisimba alisema maisha ya uraiani yana changamoto nyingi hivyo utaratibu ubadilishwe na wafungwa hawa wawe wanajengewa uwezo wa kijasiriamali.
Alitoa mfano kwa watumishi walioajiriwa; iwe serikalini au kwenye kampuni binafsi ambao hupoteza maisha muda mfupi baada ya kustaafu. “Zamani walikuwa wanapewa mafunzo na vitendea kazi. Wakija uraiani wanajiajiri kulingana na mafunzo waliyoyapata,” alisema.
Na Julius Mnganga, Mwananchi