BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kwa sasa mfumo wake wa kiutendaji uko imara, huku likieleza kuwa hakuna mbinu wala mkakati wowote wa kumpindua Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir (pichani).
Hayo yamesemwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Taifa na Msemaji rasmi wa Bakwata, Shehe Khamis Mataka kutokana na taarifa zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinamtuhumu Mufti na pia kudai kuwa kuna mbinu za kutaka kumpindua, jambo ambalo amesema halina ukweli.
Shehe Mataka alisema katika siku za karibuni kumejitokeza kadhia tatu zinazolihusisha baraza hilo na kiongozi wake mkuu, Shehe Zubeir, ambazo alisema si sahihi zikidai kuwa kuna tishio la kumuondoa Mufti, wafanyakazi wa Bakwata kulia njaa na mgogoro wa walimu wa Shule ya Sekondari Bondeni jijini Arusha inayomilikiwa na baraza hilo.
Akifafanua kuhusu tishio la kumuondoa Mufti, Shehe Mataka alisema habari hiyo chanzo chake ni mitandao ya kijamii na aliyeandika habari hizo, amedai kuwepo kwa mgogoro unaowahusisha baadhi ya wajumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, wajumbe wa Halmashauri Kuu na mashehe wa mikoa ya Dar es Salaam na Tabora na kwamba kuna njama za kumuondoa Mufti madarakani kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa mali na kushindwa kuliongoza baraza hilo.
“Bakwata Makao Makuu inapenda kuufahamisha umma wa Waislamu na Watanzania kwa ujumla habari hiyo haina mashiko na ni uzushi na uongo mweupe unaolenga kulivuruga baraza.
Hakuna njama zozote za kumuondoa Mufti madarakani. Hakuna ubadhirifu wowote unaotuhumiwa nao na kwa hakika ni kuwa hakuna kipindi chochote ambacho baraza limeimarika na kufanya mambo yake kwa mujibu wa Katiba yake kuliko kipindi hiki cha uongozi wa Mufti,” alisema Shehe Mataka na kuongeza:
“Kwa sasa tuko imara kimfumo na kikatiba na tunakumbuka huko nyuma kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2016, Bakwata ilishindwa kuitishia Mkutano wa Baraza Kuu, lakini chini ya uongozi wake amefanikiwa na wajumbe walioshiriki hakuna ambaye alipewa posho zaidi ya kutumia fedha zao.
Haya ni mabadiliko makubwa kimfumo na wajumbe wa baraza hilo wanamuunga mkono kwa hatua anayofanya.” Alitumia nafasi hiyo kuiambia jamii kutumia vyema neema ya maendeleo ya kiteknolojia badala ya kuitumia vibaya na kujaribu kuvunja heshima za watu kwa madai ya uongo na kueneza fitina katika jamii.
“Bakwata kwa kushirikiana na vyombo vya mamlaka husika, ikiwamo TCRA, itafuatilia kwa karibu suala hili lililolenga kuchafua heshima ya Mufti na taswira ya baraza kwa ujumla,” aliongeza.
Aliongeza kuwa baraza linasimamia kwa dhati falsafa ya Mufti ya ‘Jitambue, Badilika, Acha mazoea’ katika kusimamia mabadiliko ya kimfumo na kiuendeshaji ndani ya baraza na wale wote watakaobainika kukwaza juhudi hizo kwa kuzusha fitina na kula njama ya kulivuruga nafasi zao katika baraza au katika jamii.
Akizungumzia malimbikizo ya mishahara wa wafanyakazi wa makao makuu, alikiri ni kweli na Sh milioni 176 zinadaiwa, lakini wanaendelea kulipa kwani ni malimbikizo ya muda mrefu na yalifanywa na waliotangulia ofisini.
Kuhusu mgogoro wa walimu katika Sekondari ya Bondeni Arusha, Shehe Mataka alisema ni kweli kulikuwa na matatizo kwenye malipo, lakini wamemaliza mgogoro huo na mambo yanakwenda vema.
Akifafanua alidai kuna baadhi ya watu waliokuwa kwenye nafasi na sasa wamewekwa nje kutokana na mabadiliko ya mfumo, baadhi wamekuwa chanzo cha kueneza taarifa za uzushi kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuichafua Bakwata.
IMEANDIKWA NA OSCAR JOB - HABARILEO
Social Plugin