Dkt. Louis Shika ambaye amejipatia umaarufu baada ya kutangaza dau la kununua nyumba za Lugumi, amesema kwamba hivi karibuni anatarajia kwenda kuishi Marekani, baada ya Umoja wa Mataifa kumpandisha cheo.
Akizungumza kwenye kipindi cha Weekend Breakfast cha East Africa Radio, Dkt. Shika amesema awali alikuwa anafanya kazi kwenye shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi (UNHCR) na sasa amepandishwa cheo, hivyo hata ofisi zake hazitakuwa tena Nairobi nchini Kenya, kwani zitahamishiwa New York Marekani.
“Sasa hivi nina mpango wa kusajili kampuni yangu halafu mimi nisepe, nikiwa hapa nchini nanyanyasika, nilikuwa nafanya kazi na Umoja wa Mataifa Bara la Afrika, sasa ni world wide, ofisi itakuwa New York, nimepandishwa cheo, nafaya kazi ofisi ya UNHCR.
“Hata mama Kevela alipogundua mimi ni balozi akasema nyinyi ndio mnaoongoza nchi hii, na watu wajue kuwa uteuzi wangu haukutokea Tanzania, nimeteuliwa kwa veto power, hizi ziko tano kwenye umoja wa mataifa, jina langu lilikuwa projected na Urusi na mwenyewe Rais Vladimir Putin”, amesema Dkt. Shika.
Dkt. Shika ameendelea kwa kusema kwamba kura ambazo alipata zilitosha kwa yeye kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa, kwani nchi tatu zilikubali jina lake kupitishwa ikiwemo na Marekani.
Social Plugin