HII NDIYO JEURI YA CCM - DR SHEIN


MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema CCM ina uzoefu mkubwa wa kufanya mageuzi ya kifi kra, itikadi, sera na mabadiliko mengine ya kimaendeleo kwa kufuata matakwa ya wananchi bila ya kuathiri misingi imara iliyoachwa na waasisi.


Alisema hayo jana katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja ulioenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa mkoa huo kichama Marumbi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ambao Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan alihudhuria.

Dk Shein alisema CCM si chama cha mtu mmoja kama vingine vinavyoendelea kupoteza mwelekeo na kusambaratika hivi sasa kwa kukosa uzoefu wa historia kama ilivyo kwa CCM. Dk Shein ambaye mkoa huo ndiyo wake kichama, alisema ni vyema wajumbe wa mkutano huo wakatambua hivyo na kuhakikisha viongozi watakaowachagua wanaielewa itikadi ya chama hicho na sera zake na kuwa tayari kuzilinda, kuzisimamia na kuzitekeleza kwa vitendo.

Alisema viongozi watakaochaguliwa watalazimika kuwa tayari kuwakemea na kupambana na wazembe, wababaishaji, wabinafsi na wenye tabia ya kufanya kazi kwa mazoea. Aliwataka viongozi hao kuwa makini kwani umakini wao katika uchaguzi wa viongozi na kukemea maovu ndiyo unaokipa chama hicho nguvu zaidi za kukubalika, kuchagulika na kupendwa.

“Chama chetu kinapendwa na kinawavutia wananchi na kina uwezo mkubwa na wa pekee wa kurejesha na kujenga matumaini mapya kwa wanachama wake na wananchi hivyo hapana shaka tuna nafasi nzuri ya kuendelea kushika dola kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dahari na zama nyingi zijazo,” alisisitiza Rais Dk Shein.

Alisema ushindi wa kishindo ambao CCM imepata katika Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika kata 43 za mikoa 19 ya Tanzania Bara, ni ithibati ya kwamba CCM ilipitisha viongozi wenye sifa, uwezo, nia njema na waliokubalika kwa wananchi katika kugombea nafasi hizo.

Alisema ushindi mkubwa uliopatikana maeneo ambayo wapinzani walidhani ni ngome zao ni uthibitisho kuwa wananchi wanaendelea kukiamini na kukipenda chama hicho na maendeleo ya dhati ya nchi yamo ndani ya CCM inayosimamia vyema amani na utulivu uliopo nchini.

Aliupongeza mkoa huo kwa kutekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kwa kushirikiana na Serikali ambapo mafanikio yamepatikana katika sekta za uchumi na kijamii. Pia aliwasihi viongozi wote ambao kura zao hazitatosha, wasivunjike moyo na watambue mshindi ni CCM na akawasihi viongozi watakaochaguliwa kusimamia majukumu yao vizuri.

Makamu wa Rais, Samia ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alitoa salamu za Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk John Magufuli na kusisitiza wajumbe wa mkutano huo kuwachagua viongozi watakaoimarisha zaidi chama hicho ili kiendelee kupata ushindi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Juma Abdalla Sadallah “Mabodi” alitoa salamu za chama akisema kimekuwa imara na viongozi waliochaguliwa na watakaochaguliwa katika mkutano huo ni weledi na watakipeleka katika ushindi mkubwa wa Uchaguzi Mkuu 2020.
Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post