WAKATI kukiwa na dhana potofu kuwa baadhi ya wanaume wa Jiji la Dar es Salaam, ndio wanaopungukiwa zaidi na sifa za kuwa wanaume halisi kutokana na maisha wanayoishi, imebainika kuwa hivi sasa kuna kesi pia zinazothibitisha baadhi ya wanaume katika mikoa mbalimbali nchini, wanakabiliwa na matatizo ya uzazi.
Imebainika pia kuwa uhaba wa wataalamu wa tiba wa magonjwa ya uzazi kwa wanaume nchini, unaathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa tiba sahihi ya magonjwa hayo ya uzazi yanayowakabili wanaume,ambayo yanazidi kuongezeka kwa kasi hivi sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Hayo yalibainishwa na Mtaalamu wa Tiba ya Uzazi Mbobezi kwenye Tiba ya Uzazi Kwa Wanaume, Dk Yahaya Kapona alipofanya mahojiano maalumu na gazeti la Habarileo jijini Dar es Salaam jana.
Dk Kapona ni daktari mstaafu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, na hivi sasa anamiliki hospitali yake iitwayo Tikaya iliyopo Chanika Buyuni wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, ambayo imebobea katika upimaji wa afya ya uzazi kwa wanaume.
Mtaalamu huyo alisema wanaume wengi wenye matatizo ya uzazi waliofika katika hospitali yake kutoka katika maeneo mbalimbali nchini, wamebainika kuwa na moja ya kasoro katika viungo vya uzazi, ambazo kwa kiwango kikubwa zinasababishwa na aina ya vyakula wanavyokula na mabadiliko ya mfumo wa maisha.
“Si wanaume wa Dar tu kama ambavyo hivi sasa inavumishwa kuwa ndio wanakabiliwa zaidi na matatizo ya uzazi, bali wanaume katika maeneo mbalimbali nchini wanafika hapa katika hospitali yangu wakiwa na matatizo ya uzazi na tunapowafanyia uchunguzi wa kina tunabaini ni kweli wana matatizo yanayoathiri uzazi,” anasema Dk Kapona.
Akizungumzia kiundani kuhusu namna wanaume wanaofika hospitalini hapo kutoka katika mikoa mbalimbali nchini, Dk Kapona alisema wanaume hao hupimwa uwezo wa mbegu za uzazi.
“Kuna vitu vitatu ndani ya mbegu za wanaume ndivyo vinavyopimwa, unajua kwa kawaida mbegu ya mwanaume ina sehemu kubwa tatu ambazo ni mkia, kichwa na eneo la katikati,” anasema.
Alisema sehemu hiyo ya mbegu, inatakiwa kuwa na sifa stahiki isiyozidi wala kupungua kiwango kinachohitajika na kwamba kama mojawapo ya sehemu hizo ina kasoro, mwanaume husika hushindwa kumpa mimba mwanamke.
Alisema kwa wanaume wanaofika katika hospitali hiyo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar, Dar es Salaam na mikoa mbalimbali, wamekuwa wanapimwa na kubainika kuwa na kasoro moja au mbili katika sehemu hizo tatu za mbegu.
Alisema, tiba ya magonjwa ya uzazi kwa wanaume, inahitaji zaidi mtaalamu aliyejikita zaidi kwenye tiba za aina hiyo, ambaye anaweza kutumia muda wake mwingi kutafiti changamoto za tiba za uzazi kwa wanaume na kuja na tiba mbadala, ambapo alikiri kukosekana kwa wataalamu hao.
Alisema mtaalamu huwa na jukumu la kupima mbegu za mwanaume kwa muda stahiki na kwa vifaa maalum kwa ajili ya kazi hiyo, kitu ambacho alidai kuwa kwa hapa nchini hakuna huduma ya kisasa ya upimaji wa mbegu za kiume na wataalamu wa kutosha wa kazi hiyo.
“Kwa nchi za wenzetu kama vile Ugiriki ambapo nilisomea fani hii ya tiba za magonjwa ya uzazi kwa wanaume, kuna watalaamu wabobezi kwenye tiba za magonjwa ya uzazi kwa wanaume. Hiyo inafanya kuwepo kwa vifaa maalumu na vya kisasa vya tiba za uzazi kwa wanaume na pia utaalamu wa tiba hizo,” alisema.
Alisema, kutokana na uhaba wa wataalamu hao nchini, hivi saa ni kawaida kukuta madaktari mabingwa wa magonjwa ya uzazi kwa wanawake, ndio haohao wanatoa matibabu kwa wanaume wenye matatizo ya uzazi, jambo ambalo alisema si sahihi kutokana na unyeti wa suala husika.
“Ilipaswa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) kuwepo na Kitivo cha Mafunzo ya Tiba za Magonjwa ya Uzazi kwa Wanaume, lengo likiwa ni kuja kuzalisha wataalamu watakaosaidia kukabiliana changamoto za uzazi kwa wanaume,” alisema Dk Kapona.
Gazeti la Habarileo pia lilizungumza na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Obadia Nyongole ambaye alikiri kukosekana kwa wataalamu wa tiba za aina hiyo hapa nchini, huku akiweka wazi kuwa kwa ujumla kuna uhaba wa madaktari wa fani mbalimbali.
Alisema MAT inaendelea na mkakati utakaosaidia upatikanaji wa madaktari bingwa na kwa kuanzia imeanza mchakato wa kuwakata Sh 5,000 madaktari katika mishahara yao ili zitumike kuchangia kusomesha madaktari bingwa nchini.
“Ni kweli kuna uhaba wa madaktari bingwa wa magonjwa ya uzazi kwa wanaume, changamoto hiyo ni kwenye magonjwa mengine pia na hivyo MAT tunakabiliana na hilo kwa kushirikiana na serikali ili na yenyewe ikisomesha na sisi pia tusomeshe,” alisema Dk Nyongole.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammed Bakari alisema kuwa madaktari wa tiba za uzazi, wanaotibu matatizo ya uzazi kwa wanawake, ndio haohao wamefundishwa na ndio wana uwezo wa kutibu wanaume pia.
Imeandikwa na Evance Ng'ingo - Habarileo