Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Simon Haule akionesha Laptop,simu na bunduki iliyoporwa na jambazi aliyeuawa kwa kupigwa risasi - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni jambazi aliyejulikana kwa jina la Bahati Peter maarufu 'Chata' (28) mkazi wa Old Shinyanga amefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari polisi mkoa wa Shinyanga wakati akiwatoroka akiwa chini ya ulinzi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Desemba 21,2017 Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule alisema kijana huyo alifariki dunia Desemba 19,2017 saa nne na nusu usiku wakati anakimbizwa hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari.
“Chanzo cha tukio hilo ni Bahati Peter kutaka kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari wakati akiwapeleka askari hao kuwaonesha washirika wenzake wa ujambazi baada ya kukamatwa na silaha aina ya shortgun yenye namba 006096210 TZ CAR 98454 ikiwa na risasi nne iliyokuwa imefichwa shambani”,alieleza kamanda Haule.
“Bunduki hii ni mali ya kampuni ya ulinzi ya Unity Security iliyoporwa na marehemu akishikiana na wenzake baada ya kumjeruhi mlinzi wa Unity Security Sospeter Richard (30) aliyekuwa analinda kwa Wachina wanaojishughulisha na kuchezesha bahati nasibu tarehe 17.12.2017”,alifafanua kamanda Haule.
Hata hivyo alisema awali marehemu baada ya kupekuliwa alikuwa na laptop aina ya HP,simu aina ya Samsung zote zikiwa na thamani ya shilingi milioni 2 zilizoibiwa eneo la Klabu ya Burudani ya Level Four katika jengo la NSSF Shinyanga.
“Marehemu ambaye pia aliwahi kufungwa jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na kuachiwa gerezani mwezi Novemba mwaka huu kwa rufaa,tulipomhoji kwa kina alikiri kufanya matukio ya ujambazi katika mkoa wa Shinyanga na mikoa ya jirani”,aliongeza kamanda Haule.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na juhudi za kuwatafuta na kuwakamata washirika wenzake wa ujambazi zinaendelea.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na polisi na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi mapema hasa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka.
Aliongeza kuwa jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu na kuwataka wamiliki wa sehemu za starehe hasa kumbi za starehe wafuate masharti ya leseni zao.
Imeandikwa na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Imeandikwa na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha bunduki aina ya shortgun iliyoporwa na jambazi huyo
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha nguo ya kuficha uso iliyokuwa inatumiwa na jambazi huyo
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu tukio la kuuawa kwa jambazi
Waandishi wa habari wakiwa katika ukumbi wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin