MAHAKAMA ya Wilaya ya Chato mkoani Geita imemhukumu mkazi wa kijiji cha Kalema, Lukasi Nzoma (44), kwenda gerezani miaka mitatu au kulipa faini ya Sh. 200,000 baada ya kupatikana na hatia ya kumshawishi hakimu wa mahakama hiyo hongo ya kuku mwenye thamani ya Sh. 15,000.
Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Hakimu Jovitha Kato wa Mahakama ya Wilaya ya Chato, baada ya mshtakiwa Nzoma kukiri kutenda makosa mawili kabla hata ya kufikiwa hatua ya kuanza usikilizaji wa kesi hiyo.
Makosa hayo ni kushawishi na kutoa rushwa.
Mshtakiwa alikiri mara tu aliposomewa mashtaka hayo katika hatua ya kutajwa kwa ajili ya kupangiwa hakimu wa kuisikiliza.
Ndipo Hakimu Kato alipolazimika kuitolea hukumu kwa kumuamuru kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. 200,000.
Awali, mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Augustino Mtaki alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Kato kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 21, mwaka jana.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa Nzoma alimshawishi Hakimu Kato kumpatia kuku mwenye thamani ya Sh. 15,000 kama rushwa ili aweze kumpatia upendeleo katika kesi iliyokuwa mbele yake.
Kesi hiyo iliyomhusu mshitakiwa Nzoma na mkewe, ilikuwa ya mgogoro wa ndoa.
Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujietetea, alidai yeye ni mgonjwa na ana familia inayomtegemea hivyo akaiomba mahakama imuonee huruma.
Alinusurika kwenda gerezani baada ya kulipa faini.
Akizungumzia hukumu hiyo juzi, Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Chato, Vangisada Mkalimoto alitaka wananchi kujiepusha na vitendo vya kushawishi na kutoa rushwa.