Spika wa Bunge, Job Ndugai ametoa sababu zilizomfanya ashindwe kwenda kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Spika huyo, ambaye amelaumiwa na Lissu kwa kushindwa kumjulia hali, amesema hali ya sintofahamu iliyojitokeza nchini humo baada ya uchaguzi mkuu ilikuwa kikwazo kwake.
Akizungumza jana na waandishi wa habari nyumbani kwake Kisasa mjini hapa, Ndugai alisema sintofahamu hiyo ilisababisha baadhi ya wanasiasa kwenda mahakamani hivyo kufanya uchaguzi mkuu kurudiwa na kusababisha malumbano yaliyofanya kuwa na ‘Serikali kama ya mpito’.
Alisema wabunge wanaweza kwenda Kenya kama wanavyotaka ilimradi wawe na hati ya kusafiria, lakini yeye hawezi kufanya hivyo.
“Ninapokwenda kule lazima kuwe na taarifa rasmi za kiserikali na za kibunge na ninapokelewa kihivyo. Na ninapopelekwa huko hospitali ama wapi napelekwa kwa namna hiyo ndio utaratibu wa nchi kwa nchi,” alisema.
“Haiwezekani wao wana vurugu mechi kama zile halafu Spika anaonekana anazungukazunguka Nairobi, wanaweza kusema ajenda alikuja nayo si hii katika pande hizi mbili, Watanzania wamemtuma ajenda yake. Unapokuwa kiongozi lazima ujiongeze, haukuwa wakati mzuri wa Spika kwenda (Nairobi).”
Alisema kwa sababu mambo hayo yamepita na Serikali imeshapatikana basi Watanzania wangoje Krismasi na Mwaka Mpya upite na kwamba baada ya hapo watamuona akienda kumjulia hali Lissu ambaye amelazwa tangu Septemba 7 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 32 nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma.
“Ni mbunge wetu, tunampenda na tuko naye na tusingependa asikitike kwa lolote lile,”alisema Ndugai.
Alisema alishatuma wabunge wawili ambao ni Mary Chatanda (Korogwe Mjini –CCM) na Faharia Khamis Shomari (Viti Maalumu-CCM) kwa niaba ya Bunge kwenda kumuona Lissu.
Hata hivyo, Lissu katika mahojiano yake na Mwananchi hivi karibuni alisema wabunge hao walikwenda kibinafsi.
“Mmoja kutoka Bara (Mary) na mwingine kutoka Zanzibar (Faharia) wote wanawake hawa ni wajumbe wa Kamisheni ya Bunge ama Tume ya Huduma za Bunge, wabunge watatu pamoja na ofisa mwanadamizi wa Bunge kwenda kule hospitalini Nairobi, wakamtembelea na wakampa salamu zetu na tume ndio inayohusika na maslahi yote ya wabunge,” alisema.
Alisema kuwa tume hiyo ambayo ina wajumbe wachache ndio inayohusika na mbunge akifariki, ugonjwa na kwamba ndio mwajiri wa wabunge.
“Kwa kweli tulipeleka uwakilishi wa kwenda kumuona mwenzetu, akisema hajawaona watu haina tatizo unajua mtu ukiwa unaumwa unaweza mambo mengine yakakupita kidogo, kwa hiyo tuko karibu sana na jambo hili tuko naye yamesemwa mengi kuhusu Bunge tuna majibu ya kila moja,” alisema.
Kuhusu haki za Lissu, Ndugai alisema yupo kimya kwa sababu kujibishana na mgonjwa haipendezi na kwamba hata kama mgonjwa anakosea hawawezi kubishana naye.
“Hii inanipa kazi sana, nilishatoa ushauri kwao kimya kimya kuwa mambo ya kiserikali na kibunge huwa yanaenda kwa makaratasi, hayaendi kwa kuzungumza na waandishi wa habari, walichotakiwa kuandika hicho ambacho Bunge tunaambiwa kuwa hatukitekelezi,” alisema.
Alisema kwa kuandika unachokitaka kwa vyovyote vile ni lazima utapata majibu kwa maandishi ya kuhusiana na jambo hilo kama liko sawa sawa ama la.
“Utaratibu uliotumika wa kumpeleka Lissu Nairobi hatuulaumu wala nini lakini ulikuwa ni utaratibu kidogo unakwenda kushoto tofauti na utaratibu wa kiserikali na kibunge yaani utaratibu huo ni wa mimi na nyinyi nyote Watanzania,” alisema.
Alisema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndio itakayotoa rufaa kwenda kokote unapokwenda na wengi tunapelekwa India ikiwemo mimi.
Alisema kama huwapati chanzo inakuwa ni vigumu sana wakati ndani ya nchi kuna michakato ya kupitia ili kuweza kufikia jambo hilo.
Alisema jambo hilo haliamuliwi na yeye mwenyewe na kwamba ni jambo linahitaji mchakato na ni lazima alipeleke kwa wataalamu wa afya ambao wataona kama kwenda Nairobi kumuangalia na kuleta nchini mapendekezo ya kulitatua kama Mtanzania (Lissu) mwenye haki zake.
“Narudia tena jambo hili halitatuliki kwa kulaumu kwenye vyombo vya habari wala kufanya vinginevyo iwe kwa kiongozi wa upinzani bungeni ambaye mara nyingi ameongea na waandishi wa habari akinilaumu. Kwa nini asishike dokezo akaona wapi limekwamia,” alisema.
Na Sharon Sauwa- Mwananchi Dodoma
Social Plugin