Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kimenuka !! WAZIRI MKUU APULIZA JIPU UPOTEVU MALI ZA SHIRECU NA NYANZA...AAGIZA VIGOGO 19 KUJIELEZA,MAJINA YOTE HAYA HAPA


Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa ya Shinyanga (Shinyanga Region Cooperative Union - SHIRECU) na Mwanza (Nyanza Cooperative Unioni - NCU) wampe maelezo yatakayomridhisha juu ya mahali zilipo mali za vyama hivyo viwili na kuyawasilisha katika ofisi ya Waziri Mkuu Januari 13,2017.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo Ijumaa Desemba 22,2017 wakati wa kikao cha wadau wa pamba kutoka mikoa 16 nchini kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Savannah Plains mjini Shinyanga.

Viongozi hao wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama hivyo vya ushirika. 

“Nataka kila mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” alisema Waziri Mkuu. 

“Hawa nitakaowataja walipaswa kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na hatua dhidi yao zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma ifikapo Januari 15, 2018 saa 3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisisitiza. 

Kuhusu tuhuma za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza Cooperative Union - NCU), Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka 2001 na 2017, kilikuwa jumla ya mali 10 ambazo ziliuzwa kinyemela katika mazingira yenye utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani halisi ya mali hizo zilizopo jijini Mwanza. 

Aliwataja viongozi waliohusika na upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Murtazar Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU, Bw. Samson Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills), Bw. Amos Njite Lili (mnunuzi wa ghala la Igogo), Bi. Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills), Bw. Peter Ng’hingi (aliyekuwa Mjumbe wa Bodi), Bw. Daniel Lugwisha (aliyekuwa Mhasibu Mkuu - NCU), Bw. George Makungwi (aliyekuwa Afisa Miliki - NCU) na Bw. Sospeter Ndoli (aliyekuwa Afisa Utumishi -NCU). 

Kuhusu mali za Nyanza zinazoshikiliwa na benki ya CRDB,Waziri Mkuu alisema benki hiyo inaidai NCU mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 2.123 na kwamba benki hiyo inashikilia mali 16 zenye thamani ya sh. bilioni 18.132. Alitaka vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa mikopo na mali zinazoshikiliwa na benki ya CRDB. 

Kwa upande wa viongozi wa SHIRECU, Waziri Mkuu alisema wanatuhumiwa kwa upotevu wa zaidi ya sh. bilioni 11 ambazo wanadaiwa na benki ya TIB yakiwemo madeni ya mishahara ya watumishi ambayo yanafikia sh. bilioni 1.2. 

“SHIRECU kwa sasa haina mali zozote kwa sababu mali zote zinashikiliwa na TIB kutokana na mikopo,” alisema. 

Aliwataja viongozi wa SHIRECU ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Bw. Joseph Mihangwa (Meneja Mkuu), Bw. Sillu Mbogo (Kaimu Mhasibu Mkuu), Bw. Maduhu Nkamakazi (Kaimu Mkaguzi wa Ndani), Bw. James Kusekwa (Kaimu Meneja Uendeshaji) na wajumbe wa Bodi ya SHIRECU. 

Wajumbe hao wa Bodi ni Bw. Robert Mayongela (Mwenyekiti), Bi. Mary Mabuga (Makamu Mwenyekiti), Bw. Sigu Maganda (Mjumbe), Bw. Clement Bujiku (Mjumbe) na Bw. Charles Lujiga.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili mkoani Shinyanga leo asubuhi, alikwenda kwanza kukagua kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha JOC na kisha kurejea ukumbini kuendelea na kikao cha wadau wa pamba ambacho kimeshirikisha wakuu wa mikoa 16, wabunge, ma-RAS, wakuu wa wilaya, wakulima, wanunuzi wa pamba na wenye viwanda.


MSIKILIZE HAPA WAZIRI MKUU AKIZUNGUMZIA KUHUSU KUPOTEA KWA MALI ZA NYANZA NA SHIRECU NA KUTOA MAAGIZO KWA WALIOHUSIKA



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwaagiza viongozi wa Nyanza na SHIRECU kuandika maelezo kuhusu mali za vyama hivyo vya ushirika - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Baadhi ya viongozi wa SHIRECU wakiwa wamesimama wakati waziri mkuu akitoa agizo
Wadau wa pamba wakiwa ukumbini

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com