Mwaka 2004 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya na watoto wake watatu ambao ni Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto.
Kesi hiyo ilivuta hisia za watanzania wengi kutokana na umaarufu wa wasanii hao na kuhusika kwa familia nzima katika makosa mazito kama hayo. Rufaa mbali mbali zilikatwa na mawakili maarifu nchini lakini hawakuweza kuwatoa wasanii hao.
Mwaka 2010, rufaa yao nyingine ilisikilizwa katika Mahakama ya Rufaa, na kuwaachia huru Nguza Mbangu na Francis Nguza baada ya kuwaona hawana hatia katika makosa yote waliyoshitakiwa.
Baada ya rufaa hiyo, Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela. Tarehe 30 Oktoba 2013, Mahakama ya Rufaa iliyoketi chini ya jopo la majaji watu, likiongozwa na Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati walisikiliza hoja za pande zote kuhusu ombi la kufanyika mapitio ya uamuzi wa awali wa mahakama hiyo.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili wao Mabere Marando uliomba kupitiwa upya kwa uamuzi huo, ukidai kuwepo kasoro katika ushahidi uliowatia hatiani, ikiwemo kukosekana kwa mashahidi muhimu katika kesi hiyo.
Majaji walisema kuwa kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003. Kesi hiyo iliwashtua mashabiki wa mwanamuziki Nguza Viking nchini Tanzania na ukanda mzima ya Afrika Mashariki. Mwanamuziki huyo ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi Tanzania kwa miaka mingi na kuwa na mashabiki wengi.
Siku zote walipofikishwa mahakamani walionekana kuwa watulivu hata wakati majaji walipotupilia mbali ombi lao kutaka hukumu yao kubatilishwa. Juni 25, 2004 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu, Dar es Salaam,iliwatia hatiani Babu Seya na wanawe ‘Papii Kocha’, Nguza Mbangu na Francis Nguza kwa kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti.
Januari 27 mwaka 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya ambaye aliwatia hatiani kwa makosa yote waliyokuwa wameshitakiwa nayo Juni 25 mwaka 2004.
Babu Seya na wanawe walidaiwa kutenda makosa 10 ya kubaka watoto wa Shule ya Msingi Mashujaa wenye umri kati ya miaka sita na minane na makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri huo huo kati ya April na Oktoba 2003 katika maeneo ya Sinza kwa Remmy wilayani KinondonI Dar es Salaam.
Via>>Habarileo