MWANAMKE Asha Mashaka (27), mkazi wa Msamvu B, Kata ya Kihonda Maghorofani, Manispaa ya Morogoro amejifungua kwa njia ya upasuaji watoto wanne pacha.
Kati ya watoto hao, wawili ni wa kike na wawili wa kiume ukiwa ni uzazi wake wa tatu tangu aolewe na Rajab Mkwanda (31), mkazi wa Kilosa Mbuyuni, mkoani Morogoro na hivyo kufikisha idadi ya watoto sita.
Ofisa Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Grace Mulale alisema kuwa, Asha alifanyiwa upasuaji huo Desemba 18, mwaka huu katika hospitali hiyo. Mulale alisema kuwa walimpokea Asha akiwa mjamzito na walimpomchunguza waligundua kuwa hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida isipokuwa kwa upasuaji na walimpeleka kwenye chumba cha upasuaji ili afanyiwe upasuaji huo na madaktari.
Alisema alifanyiwa upasuaji na madaktari ambapo walipatikana watoto wanne ambao ni pacha, wawili wakiwa ni wa kike na wawili wa kume wote wakiwa na afya njema pamoja na mama yao.
Naye Muuguzi wa Wodi ya Watoto katika hospitali hiyo, Rehema Nyunguchi alisema baada ya kufanyiwa upasuaji na kupata watoto hao wanne, wote walikuwa chini ya uzito wa kilogramu mbili na kuhitajika wawekwe katika chumba maalumu cha joto ili kuwaongezea ukuaji.
Kwa upande wake mama wa watoto hao, akizungumza na gazeti hili alisema, huo ni uzazi wake wa tatu na kwamba uzao wa kwanza na wa pili alijifungua kwa njia ya kawaida mtoto mmoja mmoja na wote hao ni wa kike, lakini uzazi alioupata Desemba 18, mwaka huu ni tofauti kwani alifanyiwa upasuaji na kupata watoto wanne pacha.
Alisema kwa sasa anao watoto sita, wanne ni wa kike na wawili wa kiume na kutokana na kupata pacha hao aliwaomba wasamaria kumsaidia kifedha ili aweza kutunza watoto wake kwa vile yeye na mumewe hawana kazi inayowaingizia kipato cha kutosha ingawa ni wakulima wadogo wa kilimo cha kijikimu cha mboga.
“Ninawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie kwa hali na mali ikiwemo fedha zitakazonisaidia kuwanunulia maziwa watoto hawa pamoja na mahitaji mengine muhimu kwani mimi na mume wangu hatuna uwezo wa kifedha wa kuwalea watoto hawa,” alisema Asha.
Aliwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa huo kwa kutoa huduma ya haraka kwake baada ya kubaini kuwa hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida bali ni kwa upasuaji na kupata watoto hao wakiwa salama na yenye mwenyewe.
IMEANDIKWA NA JOHN NDITI- HABARILEO MOROGORO
Social Plugin