Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli ameunda tume ya watu tisa kufuatilia mali za chama hicho, akiifananisha na tume aliyoiunda kuchunguza biashara ya madini nchini.
Miongoni mwa wajumbe wa tume hiyo itakayoongozwa na Dk Bashiru Ali Kakurwa, ni kada mpya wa chama hicho, Albert Msando aliyejiunga na CCM Novemba 21 akitokea ACT-Wazalendo.
Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo leo Jumatano Desemba 20,2017 mjini Dodoma katika kikao cha kwanza cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho kilichojadili mikakati ya kuimarisha kazi za CCM na Serikali.
Wajumbe wengine wa tume hiyo ni Walter Msigwa, Galala Wabanhu, Albert Chalamila, William Sarakikya, Komanya Kitwara, Dk Fenela Mukangara na Mariam Mangula.
"Nataka nitoe wito na Waziri Mkuu yuko hapa, hii timu itachunguza mtu yeyote awe wa Serikali au kwenye chama ili mali zote ziorodheshwe," amesema katika taarifa zilizotolewa na chama hicho.
"Hii ni tume yangu, ni kama ya makinikia ila haya ni makinikia ndani ya CCM. Nataka siku moja chama hiki kiweze kujitegemea," amesema.
Mwenyekiti huyo wa CCM amewataka Watanzania wanaoshikilia mali za chama hicho kujitokeza na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa masilahi ya CCM.
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Social Plugin