Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAUAJI YA WIVU WA MAPENZI YAONGOZA SHINYANGA.....MAUAJI YA VIKONGWE YAPUNGUA KWA 70.3 %


Imeelezwa kuwa sababu kuu ya mauaji mengi yanayotokea mkoani Shinyanga ni wivu wa kimapenzi ikifuatiwa na migogoro ya mashamba,wananchi kujichukulia sheria mkononi wanapokamata wahalifu pamoja na imani za kishirikina.

Hayo yamesemwa leo Alhamis Desemba 28,2017 na Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule (pichani kushoto) wakati akitoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu yaliyotokea mkoani humo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba mwaka huu.

Kamanda Haule alisema sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa matukio ya uhalifu mfano mauaji ni wivu wa kimapenzi ambapo vifo vingi vilivyotokea mkoani Shinyanga vimetokana na wivu wa kimapenzi.

Aidha alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba mwaka huu jumla ya matukio nane pekee ya mauaji ya vikongwe yametokea mkoani Shinyanga ukilinganisha na matukio 27 yaliyotokea mwaka 2016 hivyo matukio 19 yamepungua sawa na asilimia 70.3.

“Mwaka 2012 kulikuwa na mauaji 43 ya vikongwe,mwaka 2013,mauaji 40,2014 – 26,2015- 20,2016 – 27 na mwaka 2017 – 08 pekee hakuna tukio lolote la mauaji ya watu wenye ualbino lililotokea”,alieleza kamanda Haule.

Akizungumzia kuhusu matukio yote ya uhalifu katika mwaka 2017,alisema makosa ya jinai yalikuwa 13745,makosa ya kuwania mali ni 4781,makosa dhidi ya binadamu 5297 na makosa dhidi ya maadili ya jamii 3917.

Alisema matukio yaliyotokea mwaka 2016 ambapo makosa ya jinai yalikuwa 6731,kuwania mali 4591, makosa dhidi ya binadamu 2948,makosa dhidi ya maadili ya jamii 14,266 hivyo kumekuwa na upungufu wa makosa 796 mwaka huu.

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com