MBINU YA KUOMBA PENZI KWA KUPAPASA MIGUU YA WANAWAKE YAWAPONZA WANAUME SINGIDA
Sunday, December 31, 2017
MILA inayoendelea na
jamii ya Ihanja Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ya wanandoa kuishi nyumba
tofauti, inachangia wanaume kunyanyaswa kijinsia kwa kunyimwa haki ya tendo
la ndoa.
Mila hiyo ni kwamba,
mume anakuwa na nyumba yake na anaishi na watoto wa kiume. Mke naye anakuwa
na nyumba yake na anaishi na watoto wa kike.
Mbinu inayofanyika
kumtoa mke ili wakapeane haki ya tendo la ndoa, mume akiingia anakolala mke
wake na watoto wake wa kike, humpapasa miguuni.
Kwa vile mke anajua
akipapaswa miguuni ni kwamba anaombwa tendo la ndoa, mke huamka na kwenda
mahali walikokubaliana kufanya tendo hilo muhimu kwa ustawi wa ndoa.
Hayo yamesemwa juzi
na kundi la wanaume kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na shirika lisilo
la kiserikali la Save the Mother and Children of Central Tanzania
(SMCCT). Lengo la mkutano huo, ni kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya
ukatili wa kijinsia na ukeketaji.
Ofisa Mtendaji Kata
ya Ihanja, Hamisi Mpuma, amesema ofisi yake imekuwa ikipokea mara kwa mara
malalamiko/migogoro ya kifamilia, ambayo chanzo chake kikuu ni ukatili wa
kijinsia wa kunyimana tendo la ndoa.
Akifafanua, alisema
baadhi ya wanawake kwa sababu wanazozijua wao, wamekuwa wakitumia mwanya wa
kulala na watoto wa kike, kuwanyima tendo la ndoa wanaume zao.
“Wakifuatwa na waume
zao usiku, wanadai watoto wa kike bado hawajazidiwa na usingizi, hivyo tendo
la ndoa halitafanyika. Hali hiyo haitokei mara moja, inajirudia kwa siku
tofauti tofauti.
Unyanyasaji huo, husababisha mwanamume kuhamishia hasira kwa
watoto. Mtoto akimwomba kitu baba yake, baba yake humjibu kwa ukali, nenda
kamwambie mama yako,” alifafanua.
Kuhusu mbinu ya
kupapasa mke miguu usiku, alisema hivi karibuni aliletewa malalamiko na binti
mmoja (hakumtaja) akimlalamikia baba yake kumpapasa miguu usiku wakati
wamelala.
“Baada ya kumwita
baba huyo anayelalamikiwa na binti yake, alijitetea kwamba hakuwa na nia
mbaya kwa binti yake, isipokuwa alikuwa anataka kumwamsha mke wake ili
wakafanye tendo la ndoa. Baada ya utetezi huo, tulimwomba binti amsamehe baba
yake, kwa vile hakuwa na nia mbaya,” alisema.
Akichangia hoja hiyo,
Joseph Msukuya, alisema wakati umefika jamii ya Ihanja kubadilika na kuwa na
nyumba/chumba kimoja kwa ajili ya mume na mke tu.
“Tuachane na hii
mila, kwanza imeshapitwa na wakati na haipendezi mume unatoka usiku wa manane
kwenda kupapasa mguu wa mke wake katikati ya miguu ya watoto wa kike. Wanaume
kuweni na chumba kimoja cha kulala na kufanya mambo yenu ya kupeana haki ya
tendo la ndoa,” amesisitiza Msukuya.
Na Nathaniel Limu -Singida
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin