MCHUNGAJI na waumini wa Kanisa la The Evangelistic Assemblies of God (EAGT) mtaa wa Eden 'A' Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa, wamekesha wakimuombea marehemu wao afufuke, wakidai alikufa kwa nguvu ya giza.
Elizabeth Lwitiko (30) alifariki dunia juzi saa tatu asubuhi kutokana na matatizo ya uzazi, wakati akijifungua pacha, aliowaacha hai na wametafutiwa mlezi.
Mchungaji Jacob Lwitiko aliongoza waumini wake, kuchukua mwili wa marehemu chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga na kuiweka kwenye madhabahu ya kanisa hilo na kufanya maombezi, wakiamini kuwa huenda atafufuka.
Mchungaji Lwitiko ni kaka wa Elizabeth na aliachiwa uongozi wa kanisa hilo na kaka yake, Amos Lwitiko, mwanzilishi na kwa sasa yuko Makambako mkoani Njombe. Mwenyekiti wa Mtaa wa Edeni “A” lililopo kanisa hilo, Gerald Mwazembe alikiri kuwepo kwa mkasa huo, uliowashitua wakazi wa jirani kwani ni mara ya kwanza kutokea.
Akisimulia, alisema kuwa Elizabeth alifariki dunia saa tatu asubuhi katika Kituo cha Afya cha Mazwi mjini hapa kutokana na matatizo ya uzazi, ambapo alipungukiwa damu mwilini baada ya kujifungua salama kwa njia ya kawaida watoto pacha ambao wako hai.
“Mwili wa marehemu ulihifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, lakini waombolezaji na mchungaji wa kanisa hilo waliuchukua mwili huo wakiamini alikufa kishirikina na kwamba wakimwombea angeweza kufufuka,” alieleza.
Alisema mwili ulipofikishwa kanisani hapo, uliwekwa madhabahuni na ibada ya maombezi iliyoambatana na nyimbo na midundo ya ngoma, ilifanyika kuanzia saa sita mchana hadi usiku wa manane huku milango ikiwa imefungwa, wakiamini kuwa atafufuka.
“Ilipofika usiku wa manane niliwapigia simu Polisi ambapo askari wa kikosi cha doria walifika kanisani hapo, baada ya mazungumzo marefu waliagiza mwili wa marehemu urejeshwe na kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili usiharibike,” alieleza.
Aliongeza Polisi walishuhudia mwili wa marehemu ukiwa umewekwa madhabahuni ;huku waumini wakiupapasa, wakiomba afufuke.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo, walisema Mchungaji Lwitiko aliwaongoza kwa mara nyingine kuurejesha mwili wa marehemu ili uhifadhiwe chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa huku wakisisitiza kuwa maombezi yaliyofanyika kanisani hapo ni ya imani yao.
Majirani walieleza umati mkubwa ulifurika katika uwanja wa kanisa hilo, baada ya taarifa kuzagaa kuna marehemu anaombewa mwili wake ukiwa madhabahuni, wakiamini atafufuka.
“Lakini walioruhusiwa kuingia kanisani kwa maombezi, lazima awe muumini wa kanisa hilo na baada ya kuingia mlango wa kanisa ulikuwa ukifungwa, “ alieleza mmoja wa waumini. Mwandishi wa habari hizi alifika kanisani hapo jana asubuhi na kukuta milango imefungwa ;huku nyimbo zikiendelea kuimbwa kanisani.
Baadaye aliambatana na Mwenyekiti Mwazembe na mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten kuingia kanisani kwa mahojiano na mchungaji, lakini ndugu wa marehemu nusura wawapige, wakidai hawakukaribishwa msibani.
“Kwanza nyie nani... mmekuja kufanya nini hapa ...ondokeni mara moja ....vinginevyo nendeni hospitali mkaulize uzembe walioufanya na kusababisha kifo chake,” alifoka mmoja wa wanandugu akitishia kuwapiga.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Dk Halfany Haule alisema anafuatilia tukio hilo na atatoa taarifa baadaye.
Taarifa kutoka kanisani hapo, zilieleza msiba huo upo Kitongoji cha Bangwe mjini Sumbawanga.
IMEANDIKWA NA PETI SIYAME, SUMBAWANGA