Polisi mkoani Kilimanjaro inamshikilia mfanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PPF) kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Anitha Oswald (32).
“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370 kwa kutumia gari lake analomiliki aina ya Toyota Sienta rangi ya silva,” alisema kamanda Issah.
Kamanda Issah alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Desemba 19 akitokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo.
“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara hii”, alisema.
Kamanda huyo alisema polisi wanaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza lilipogonga mti wakati akiwakimbia askari.
Social Plugin