Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC) ASIMAMISHWA KAZI


 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu amesimamishwa kazi.


Taarifa ya kusimamishwa kazi kiongozi huyo imetolewa leo Jumamosi Desemba 16,2017 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akieleza uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.


Mchechu aliteuliwa kuliongoza shirika hilo Machi Mosi, 2010. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CBA.


Taarifa ya Dk Abbasi imesema Lukuvi amechukua uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.


Mbali na Mchechu, Lukuvi ameitaka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Huduma za Mikoa na Utawala, Raymond Mndolwa.


"Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika imesisitiza kuwa uamuzi huo unapaswa kutekelezwa kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watendaji hao," amesema.

Desemba 13, wakati Rais John Magufuli akizindua nyumba 300 za shirika hilo alieleza hujuma zinazofanywa na viongozi wa NHC, akiwemo Mchechu na Bodi ya wakurugenzi.

"Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo mengi vipo, unakuwa na shirika la kujenga nyumba wakati wewe ni mkurugenzi na ni shirika lako. Unanunua viwanja kule na wewe unakwenda unanunua maeneo unayaandikia kwa majina fulani, tukichunguza tunakuta vyako, mengine nimeyamezea kwa sababu ya kazi nzuri unayofanya," alisema Rais Magufuli.

Katika hotuba yake, Rais alimtaka Mchechu kuwa makini na watu anaofanya nao kazi kwa maelezo kuwa wapo wanaotaka nafasi yake na kutumia wajumbe wa bodi na wanasiasa kumchafua.

"Wako wanaokupiga vita kwa wivu wao, lakini na wewe saa zingine matumizi yanakuwa ya ajabu," alisema Rais.
Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com