MWANDISHI WA HABARI JOYCE MMASI WAAGWA DAR ES SALAAM




Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili wa aliyekuwa mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi, Joyce Mmasi.


Shughuli za kuaga mwili wa Joyce zimefanyika leo Jumapili Desemba 10,2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.


Ibada ya kuaga mwili iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Luis, Richard Lucas.


Mchungaji Lucas amesema maisha aliyoishi Joyce yawe fundisho kwa waliobaki duniani.


"Binadamu tuna maisha mafupi ya kuishi duniani. Joyce aliyakabidhi maisha yake kwa Yesu, hivyo hakuna shaka kuwa yuko mahali salama," amesema.


Akizungumza katika shughuli hiyo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Francis Nanai amesema Joyce alikuwa mwandishi wa habari lakini pia mjasiriamali.


"Hili ni fundisho kwetu kwamba tunahitaji kuishi maisha ya kujiongeza maana Mmasi alikuwa mwanachama mzuri wa Saccos ya Mwananchi na alitoa mawazo ambayo yamesaidia maendeleo ya Saccos na kampuni," amesema.


Baada ya mwili wa Joyce kuagwa umesafirishwa kuelekea kijijini kwao Mbokomu wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho Jumatatu Desemba 11,2017.


Joyce alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatano Desemba 6,2017 baada ya kuugua kwa muda mfupi.


Andrew Kamugisha ambaye ni mume wa Joyce alisema mkewe alifariki saa kumi usiku katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.


Alisema Joyce aligundulika kuwa na saratani ya damu. Alisema kutokana na tatizo hilo, utengenezaji wa damu ikiwemo rojorojo lililoko katika mifupa (bone marrow) na hivyo kusababisha mfumo wa chembe hai kutofanya kazi inavyotakiwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post