MWENYEKITI MPYA WA UVCCM ATEMBELEA HOTUBA YA JPM

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James amewataka vijana nchini kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Rais John Magufuli.

James alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake aliyoitoa juzi mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi kuwataka wanachama kuifanyia kazi hotuba ya mwenyekiti huyo wa CCM aliyoitoa wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa UVCCM.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma, James aliibuka mshindi kwa kupata kura 319 kati ya 583 zilizopigwa na kumwacha kwa mbali mpinzani wake, Thobias Mwesiga aliyepata kura 127.

James alitangazwa rasmi jana na msimamizi wa uchaguzi huo, William Lukuvi kuwa mshindi wa nafasi hiyo iliyokuwa ikiwaniwa na wagombea saba. Wakati akitangazwa, ulinzi ulikuwa umeimarishwa ndani ya ukumbi na mwenyekiti huyo mpya alikuwa na walinzi.

“Kama kuna kazi kubwa ya kufanya katika jumuiya yetu, basi ni kuhakikisha tunapambana na rushwa. Tunakwenda kutekeleza agizo la Rais Magufuli mara moja,” alisema James.

Ili kuhakikisha hilo linafanyika kwa vitendo, James amewaagiza viongozi wa umoja huo kuichapisha hotuba hiyo na nakala zake zisambazwe mikoani na wilayani ili waanze kutekeleza maagizo ya kiongozi huyo ikiwamo kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za jumuiya hiyo.

Katika hotuba yake juzi, Rais Magufuli alisema UVCCM imekuwa dhaifu na imegubikwa na vitendo vya rushwa ndiyo maana baada ya kuchaguliwa kwake mwaka 2015, hakupelekewa orodha ya majina ya vijana wa umoja huo kwa ajili ya kuteuliwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi serikalini hivyo kutumia mbinu zake kuwatambua.

“Ninavyozungumza hapa mwenyekiti wenu (Sadifa Juma Khamis) yuko mahabusu kwa tuhuma za rushwa. Huo ndio umoja wa vijana?...”

Alisema uelekeo ambao UVCCM ilikuwa ikienda si ule anaoufahamu wakati alipokuwa mwanachama wake, hivyo inahitaji kufanyiwa marekebisho.

Kuhusu mali za UVCCM, Rais Magufuli alisema zipo nyingi yakiwamo majengo lakini zinatumika ovyo. Alitoa mfano jengo la umoja huo lililopo Dar es Salaam ambalo haijulikani linakusanya mapato kiasi gani kwa mwaka.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema ni wakati wa bodi ya wadhamini ya UVCCM kuondoka kwa sababu haina msaada wowote kwa jumuiya hiyo.

Katika uchaguzi huo, Thabia Mwita alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti kwa kura 286 dhidi ya mpinzani wake Rashid Mohamed Rashid ambaye alipata kura 282.

Wagombea wengine waliochaguliwa ni mwakilishi wa vijana Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Dotto Nyirenda, mwakilishi wa vijana kwenda Jumuiya ya Wazazi, Amir Mkalipa na wawakilishi watatu wa Tanzania Bara kwenda Baraza Kuu la UVCCM ambao ni Rose Manumba, John Katarahiya na Secky Kasuga.

Wengine ni wawakilishi wawili wa Zanzibar kwenda Baraza Kuu la UVCCM ambao ni Nasra Haji na Abdallah Rajabu. Pia wajumbe wawili kutoka Zanzibar wanaokwenda Halmashauri Kuu ya Taifa, Abdallaghari Idrisa Juma na Maryam Mohamed Khamis.

Vilevile mkutano huo uliwachagua wajumbe wengine watatu kutoka Tanzania Bara wanaokwenda Halmashauri Kuu ambao ni Sophia Kizigo, Mussa Mwakitinya na Khadija Taya (Keisha).

MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post