Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma itatoa uamuzi wa maombi ya dhamana ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis anayekabiliwa na makosa ya rushwa Desemba 19,2017.
Uamuzi huo unatokana na upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kiapo kuzuia dhamana kwa madai ya kuvurugwa upelelezi na kuingilia uchaguzi wa UVCCM ambao ulifanyika jana Jumapili Desemba 10,2017 na leo Jumatatu Desemba 11,2017 katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo amedai Sadifa anashtakiwa kwa makosa mawili.
Katika shtaka la kwanza amedai Desemba 9,2017 katika makazi yake kwenye Kata ya Mnada mjini Dodoma akiwa mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM na muajiri wa umoja huo aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.
Sadifa katika shtaka la pili anadaiwa katika eneo hilo na siku hiyo hiyo, aliwaahidi kuwalipia usafiri wanachama wa umoja huo kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi huo.
Biswalo amesoma hati ya kiapo iliyotolewa na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga kupinga maombi ya dhamana kwa sababu endapo atapewa dhamana atavuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa vijana.
Wakili wa Utetezi, Godfrey Wasonga amepinga hoja hiyo akisema makosa aliyoshtakiwa nayo mteja wake yana dhamana na hawezi kuingilia uchaguzi kwa kuwa umeshafanyika na mshindi ametangazwa.
Kutokana na mabishano hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Emmanuel Fovo ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19,2017 kutoa nafasi ya mahakama kupitia kiapo kilicholetwa na upande wa mashtaka ili kutoa haki katika maombi ya dhamana ya mshtakiwa.
Kutokana na hilo, Sadifa amerejeshwa rumande.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi