Baada ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi ya muda mrefu na wanawake watatu kwa wakati mmoja Juma aliona sasa umefika wakati wa yeye kuoa na kwa sababu hakuwa na uwezo wa kuwaoa wanawake wote hao, alipanga kumchagua mmoja kati yao na kumfanya mke.
Shida ikaja angemchagua yupi kati ya wale? Hapa sasa ikabidi Juma aombe msaada kwa babu yake, mzee aliyepigwa na jua la siku elfu na maelfu, kikongwe aliyekula chumvi kwelikweli.
Akamuuliza ‘Babu nina wanawake watatu, nataka kumuoa mmoja wao. Nimuoe yupi?’ akimaanisha aangalie vigezo gani kabla ya kumchagua mmoja kati ya wale watatu?
Babu akamwambia hiyo mbona ni kazi rahisi sana; ‘chakufanya chukua kiasi fulani cha fedha, wagaiwe wote sawasawa, kwa nyakati tofauti kamba ambavyo hawajuani, kisha kila unayempa mueleze kwamba nataka kukuoa baada ya muda fulani, hii fedha nimekupa kwa ajili ya kujiandaa na ndoa yetu, fanyia chochote utakachoona kinafaa.
Atakayerudisha hela hiyo ikiwa imezaa, huyo ndiyo mke. Mwanamke ni akili bwana, hasa linapokuja suala la kutulia na fedha.
Juma kwa sababu anamuamini babu yake, akafanya kama alivyoagizwa. Akachukue fedha kiasi, akampatia kila moja kati ya wale watatu, akawaeleza mpango wake wa kuoa na dhumuni la kuwapa halafu akakaa akisubiri matokeo.
Wa kwanza alikwenda saluni, akaweka manywele ya bei mbaya kichwani, yale manywele ambayo unahisi yanatakiwa kuvaliwa na mchepuko wako tu, mkeo akikuomba hela akasuke unaona kama ameanza tabia ya kuchezea hela, badala aombe hayo malaki mkafyatulie tofali, anaomba akanunue maplastiki aweke kichwani.
Pesa nyingine akaingia nayo mjini, kwenye maduka makubwa makubwa ya nguo. Akafanya maneno yake, akafanya maneno yake na alipotoka alikuwa ni mpya, anawaka kupita kawaida. Akarudi kwa Juma, akamwambia ‘baby’ ile pesa uliyonitumia ndiyo imenifanya hivi. Juma akajibu umependeza.
Matumizi ya wa pili yakafanana kidogo na wa kwanza. Yeye alienda mjini, akaingia duka hili na lile, akatoka na masuruali na mashati motomoto kama ya kuendea ukweni kwa mara ya kwanza, moka zilizovuka bahari za mbali, saa za kutoka India na makorokoro yote ya kiume, akaenda kumtupia Juma, akamwambia, ‘laazizi, kwenye harusi ni lazima upendeze. Nimetumia ile hela uliyonipa kununulia hivi.’ Juma akajibu ‘Asante.’
Wa mwisho akaichukua ile pesa, akaitia kwenye biashara, akaizungusha huku na huko, kwenye vikoba na vibati na baada ya muda Fulani ikaongezeka. Akauchukua kiasi kilichoongezeka, akampelekea Juma, akamwambia; ‘mpenzi, ile pesa uliyonipa nilifanyia biashara ili itusaidie tutakapoanza maisha ya ndoa. Na hii ndiyo faida iliyopatikana mwanzo. Juma akasema vizuri sana. Mwanamke ndiyo wewe.
Basi, baada ya hapo Juma akakutana na mwanamke mwingine nje ya wale watatu, mwanamke mwenye shepu ya kibantu ile ya kukufanya uwe unajiuliza kwa nini aliyetuumba aliamua kutupa maumbile yasiyofanana—Juma akamuoa mwanamke huyo.
Na hivi ndivyo akili zetu wanaume zilivyo.
Social Plugin