Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ameishangaa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutupa ushahidi wa tuhuma za rushwa aliouwasilisha pamoja na mbunge mwenzake, Godbless Lema wa Arusha Mjini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nassari leo Desemba 18,2017 amesema aliipatia taasisi hiyo kila aina ya ushahidi, kikiwemo kifaa alichotumia kurekodi baadhi ya vikao vya kuwashawishi waliokuwa madiwani wa Chadema kuhamia CCM.
Msemaji wa Takukuru, Musa Misalaba jana Jumapili Desemba 18,2017 alisema wameshindwa kuendelea na uchunguzi kwa sababu wabunge hao waliuingilia na kuuvuruga licha ya kutahadharishwa.
"Nilipowapatia kifaa kile, wakasema wana teknolojia ya hali ya juu ku-retrieve kazi zao, muda na wakati ambao video hizo zilichukuliwa bila kukosea, teknolojia ambayo mimi pia ninayo," amesema.
Mbunge huyo amebainisha kuwa taasisi hiyo haikuona uhalisi au uongo uliopo kwenye ushahidi, badala yake wameona siasa.
"Ni kweli ilikuwa lazima waone siasa kwa sababu hata ununuzi wenyewe ulikuwa ni rushwa ya kimfumo, aina hii ya rushwa ni mbaya kama itaachwa isambae katika mfumo mzima wa siasa za nchi," amesema.
"Takukuru wanasema iliingizwa siasa, najiuliza hivi kumbe tuhuma na ushahidi wa rushwa ukiletwa na mwanasiasa hubadilika rangi."
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Social Plugin