Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) amekabidhi hundi ya shilingi Milioni 6.8 ( 6,830,000/=) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika zahanati ya kijiji cha Solwa kilichopo kata ya Solwa jimbo la Solwa mkoani Shinyanga.
Akizungumza leo Jumamosi Desemba 30,2017 wakati wa kukabidhi hundi hiyo kwa kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo,Mheshimiwa Azza alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa alipotembelea zanahati hiyo mwezi Mei mwaka huu na kukuta changamoto ya uhaba wa vyumba vya kutolea huduma za afya ikiwemo wodi ya watoto na akina mama.
“Nilifanya ziara katika zanahati hii mwezi Mei mwaka huu wakati natoa vitanda vya kujifungulia na viti vya wagonjwa,baada ya kuingia katika chumba cha akina mama nilikuta vitanda vitatu,niliguswa na jinsi akina mama walivyokuwa wanahangaika,lakini nikaambiwa wananchi wana mpango wa kujenga wodi ya watoto na akina mama,nikaahidi kuchangia mabati 20 pindi majengo yatakapofikia hatua ya upauaji”,alieleza mbunge huyo.
“Mwezi Septemba mwaka huu,Diwani wa kata ya Solwa alinitumia picha za majengo mawili yakiwa tayari kwa upauaji,nikawaza kuhusu mabati yangu 20,nikaona hayatoshi,ndipo nikaamua kuanza kutafuta watu wa kunisaidia,juzi nikapokea ujumbe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF kuwa wamekubali ombi langu na wameamua kutoa shilingi 6,830,000/= kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo moja”,alieleza mheshimiwa Azza Hilal Hamad.
Alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kununua mabati na mbao pamoja shughuli zingine katika kukamilisha ujenzi wa jengo la wodi ya akina mama katika zahanati ya Solwa iliyojengwa kwa michango ya wananchi wa kijiji cha Solwa.
“Niwapongeze sana watu wa Solwa kwa kuamua kuchangishana na kuanza ujenzi,Solwa itajengwa na Wana Solwa,hili ni jibu tosha kabisa kwamba kila kilio kina mwenyewe,mlichokifanya kinapaswa kuigwa katika maeneo mengine,niwashukuru sana pia NSSF kwa kunishika mkono ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto”,aliongeza Azza Hilal Hamad.
Hata hivyo aliwataka wananchi wa Solwa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili iwe na manufaa kwa wananchi.
Mbunge huyo alitumia fursa hiyo pia kuwakumbusha wazazi na walezi kupeleka watoto shule badala ya kuwaozesha wangali wadogo kwa tamaa ya mali huku akisisitiza kuwa urithi mzuri kwa mtoto ni elimu pekee.
“Ni marufuku kuozesha watoto wa kike wanafunzi,matokeo ya darasa saba yametoka,wote waliofaulu wapelekwe shule,waliofeli nao watafutieni kazi zingine za kufanya siyo kuwaozesha,kufeli shule siyo kufeli maisha”,aliongeza.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji Solwa,George Bushiya alisema baada ya wananchi kukerwa na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya walikubaliana kuchangishana fedha ili kujenga majengo ya wodi ya watoto na akina mama ambapo zaidi ya shilingi milioni 36 zimetumika mpaka sasa.
Naye Diwani wa kata ya Solwa Awadhi Mbaraka (CCM) alimshukuru mbunge huyo kwa misaada mbalimbali ambayo amekuwa akiitoa katika kata hiyo ikiwemo vitanda vya kujifungulia kwa akina mama na ujenzi wa jengo la zahanati ya Solwa.
“Huyu mbunge amekuwa nasi tangu mwanzo kabisa tunaanza ujenzi huu,ametuletea vitanda,viti vya wagonjwa,pia amemsaidia mtoto Salawa Mihangwa (03) aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo,sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji jijini Dar es salaam,na leo katuletea pesa kumalizia ujenzi wa wodi,mungu akubariki sana ndugu yetu Azza”,aliongeza Mbaraka.
Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri ya Shinyanga,Dk. Salim Matondo alimshukuru mbunge huyo kwa kusaidia ujenzi wa wodi ya akina mama ambapo pindi ujenzi utakapokamilika itasaidia kupunguza adha ya akina mama kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya katika hospitali ya Nindo na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Baada ya Mheshimiwa Azza Hilal Hamad kukabidhi hundi ya shilingi milioni 6.8,wananchi waliohudhuria kikao hicho kifupi waliamua kutoa michango ya papo kwa papo kumuunga mkono mbunge wao ambapo zaidi ya shilingi Milioni 3 zilipatikana huku ahadi ya mifuko ya saruji,tripu za mchanga na moram nayo ikitolewa ili kuhakikisha ujenzi wa wodi hizo mbili unakamilika haraka iwezekavyo.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Muonekano wa majengo mawili yaliyojengwa na wananchi wa kijiji cha Solwa yatakayotumika kama wodi ya watoto na akina mama katika zahanati ya Solwa iliyopo katika kijiji cha Solwa,kata ya Solwa,jimbo la Solwa mkoani Shinyanga-Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Muonekano wa majengo hayo mpaka leo Jumamosi Desemba 30,2017
Muonekano wa majengo hayo mawili
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya shilingi Milioni 6.8 ( 6,830,000/=) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika zahanati ya kijiji cha Solwa kilichopo kata ya Solwa jimbo la Solwa mkoani Shinyanga.
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akielezea kuhusu namna alivyopata shilingi 6,830,000/= kutoka mfuko wa hifadhi ya Jamii NSSF kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa wodi ya akina mama katika zahanati ya Solwa
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akiwa ameshikilia hundi ya shilingi Milioni 6.8 kabla ya kuikabidhi wa wajumbe wa kamati ya ujenzi wa majengo ya zanahati ya Solwa
Hundi iliyokabidhiwa
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akikabidhi hundi ya shilingi 6,830,000/= kwa wajumbe wa kamati ya ujenzi.Kulia ni mwenyekiti wa kamati hiyo Mussa Shibina.
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akikabidhi hundi ya shilingi 6,830,000/= kwa wajumbe wa kamati ya ujenzi
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad na viongozi mbalimbali wa kijiji na kata ya Solwa wakiingia katika jengo la wodi ya akina mama ambalo ndiyo pesa iliyotolewa itatumika kukamilisha ujenzi( kuweka mbao na mabati)
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akiwa ndani ya jengo la wodi ya akina mama
Kulia ni Muuguzi msaidizi katika zahanati ya Solwa,Dk. Mehrab Nyato akitoa maelezo kwa mbunge Azza Hilal kuhusu vyumba katika jengo hilo
Mheshimiwa Azza Hilal akisikiliza maelezo kutoka Dk. Mehrab Nyato
Mheshimiwa Azza Hilal akiuliza jambo
Mheshimiwa Azza akiendelea kutembelea majengo hayo
Diwani wa kata ya Solwa Awadh Mbaraka akizungumza wakati wa kikao cha makabidhiano ya hundi
Mwenyekiti wa CCM kata ya Solwa Leonard Malando akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema kazi anazofanya mbunge Azza Hilal zinasaidia kupunguza maswali ya kwamba viongozi wa CCM wanafanya nini katika kata hiyo
Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri ya Shinyanga,Dk. Salim Matondo akizungumza katika kikao hicho
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Mussa Shibina akizungumza katika kikao hicho
Afisa Mtendaji wa kijiji Solwa,George Bushiya akizungumza katika kikao hicho
Mzee Mwinamila Kibiongo akiimba shairi la kupongeza kazi za Mheshimiwa Azza Hilal
Mbunge Azza Hilal akicheza muziki na mmoja wa wananchi wa kijiji cha Solwa ambaye alioma awekewe wimbo wa Mama Ushauri unaomhusu Mbunge Azza Hilal
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akimsalimia mama aliyejifungua mtoto wa kike mara baada tu ya mbunge kufika katika zanahati hiyo.Mama huyo alikuwa amepewa rufaa ya kwenda kujifungulia katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga,lakini kutokana na Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri ya Shinyanga,Dk. Salim Matondo kuhudhurika kikao cha mbunge,ndiyo ikawa fursa nzuri kwa mama huyo kupewa huduma na Daktari huyo
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akiwa amembeba mtoto aliyepewa jina la "Azza"
Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akifurahia jambo baada ya kumpatia zawadi ya vitenge mama aliyejifungua mtoto wa kike katika zahanati ya Solwa.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin