Mwenyekiti
wa CCM, Rais John Magufuli amekerwa na mamlaka zinazohusika na maadili
kutochukua hatua dhidi ya wasanii wanaoimba majukwani wakiwa na mavazi
ya utupu.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne wakati akufungua mkutano mkuu wa tisa wa jumuiya ya wazazi CCM utakaofanyika kwa siku mbili mjini Dodoma.
Rais Magufuli amehoji vyombo vya habari, wasimamizi wa maadili, wizara na taasisi zinazodhibiti zimeshindwa kushughulikia maadili ya vijana.
Msingi wa kauli hiyo ilikuwa ni kumtaka kiongozi wa jumuiya hiyo atakayepatikana kuhakikisha anakwenda kusimamamia maadili ya vijana na Taifa kwa ujumla.
Rais Magufuli aliwataka wazazi hao kusimamia maadili ya Watanzania.
"Hii ni jumuiya ya wazazi lakini maadili yameanza kupotea na jumuiya ipo kwa ajili ya kukemea, mimi nimekuwa shabiki mzuri wa muziki, wanaovaa utupu ni wanawake, wanaume wanacheza wakiwa wamevaa, sana sana wataachia kifua wazi tu ili waonekane 'six pack', lakini wanawake, walio wengi wanaachia viungo vyao,”
"Jumuiya imefika wakati wa kukemea, tunawafundisha nini, je akicheza bila kuvua nguo hata furahisha wimbo? Sasa ni jukumu lenu jumuiya ya wazazi, kwa kumtanguliza Mungu kwa sababu hata Adam alipotenda dhambi alijikuta yupo uchi, lakini kwenye muziki hawajioni wako uchi na wanacheza hadharani.”
Rais Magufuli amesema wakati umefika bila kujali itikadi za vyama kuungana katika ujenzi na ulinzi wa maadiili ya Watanzania.