Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliopo katika operesheni ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Askari hao wameuawa na kikosi cha waasi cha ADF huku wengine 44 wakijeruhiwa na wawili hawajulikani walipo.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu usiku wa Desemba 8, 2017 imesema kuwa, Rais Magufuli amewatumia salamu za rambirambi kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, maafisa na askari wote wa JWTZ, familia za marehemu na Watanzania wote.
‘Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu DRC’ imesema taarifa hiyo.
Hata hivyo, Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya kutokea tulio hilo, na pia amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waendelee na majukumu yao ya kawaida.