Mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma,Kanali Hosea Ndagala akiangalia ng'ombe kutoka Burundi waliokamatwa katika kijiji cha Bukiriro kata ya Gwanumpu-Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma,Kanali Hosea Ndagala akiwa na raia wanne wa Burundi walioingia na mifugo kinyume cha sheria nchini Tanzania
Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Kanali Hosea Ndagala wamekamata ng'ombe 93 na raia wanne (wachungaji) kutoka nchi ya Burundi kwa kuingia nchini kinyume cha sheria na ng'ombe hao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya oparesheni ya kufukuza mifugo kutoka nje ya nchi iliyoingizwa kinyume na utaratibu ,mkuu huyo alisema ng'ombe hao walikamatwa katika kijiji cha Bukiriro kata ya Gwanumpu ambapo baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walikuwa wamewahifadhi.
Ndagala aliwataja raia wa Burundi wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kuwa ni Ntirampeba Gerald, Ndoayo Yusto, Myosaba Joris na Ndebe Lema.
Ng'ombe hao waliokamatwa walikuwa wamehifadhiwa kwa Bw. Gozbati Moses (ng'ombe 27) na Bw. Kaitila Mgiligiji (ng'ombe 66) wakazi wa kijiji cha Bukiriro, kata ya Gwanumpu Tarafa ya Kasanda wilayani humo.
"Niwaombe viongozi wote hususani wa vijiji vya mpakani kuwajibika na kuhakikisha kuwa hakuna mifugo yoyote kutoka nchi jirani inayoingia au kuwekeshwa kwa mtu yeyote atakayekutwa anahifadhi mifugo hiyo atachukuliwa hatua za kisheria, msigeuze nchi yetu kuwa shamba la bibi, zoezi hili ni endelevu", alisema Ndagala.
Aidha, Kanali Ndagala aliwashukuru wananchi waliotoa taarifa kufanikisha zoezi hilo na kuwataka kuendelea kutoa taarifa wanapobaini uwepo wa mifugo kutoka nje ya nchi na kuwaagiza wananchi wote wenye tabia ya kuwekeshwa mifugo kutoka nchi jirani na kuajiri wageni kinyume na taratibu kuacha mara moja.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma