Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameibwaga Serikali mahakamani, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali rufaa dhidi yake.
Serikali ilikata rufaa Mahakama Kuu Dar es Salaam, ikipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumwachia huru Sheikh Ponda katika kesi ya jinai namba 128 ya mwaka 2013.
Katika kesi hiyo, Sheikh Ponda alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro na kukaidi amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kumtaka asifanye kosa lolote katika kipindi cha miezi 12.
Hata hivyo katika hukumu yake aliyoitoa Novemba 30 Hakimu Mkazi Mary Moyo alimwachia huru Sheikh Ponda pamoja na mambo mengine akisema kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka.
Upande wa Mashtaka haukukubaliana na hukumu hiyo, hivyo ukakata rufaa Mahakama Kuu Dar es Salaam, ukiwasilisha hoja tatu za kupinga hukumu hiyo.
Pamoja na mambo mengine upande wa mashtaka ulikuwa ukidai kuwa Hakimu Moyo alikosea kumwachia huru Ponda kwa hoja kwamba upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
Mahakama Kuu katika hukumu yake imetolewa leo Desemba 18 na Jaji Edson Mkasimongwa, ilitupilia mbali hoja zote za rufaa ya Serikali na badala yake ikakubaliana na hukumu ya Mahakama ya Morogoro.
Akisoma hukumu hiyo leo Desemba 18 , Jaji Mkasimongwa amesema alikubaliana na hoja za mawakili wa mjibu rufani (Sheikh Ponda) wakiongozwa na wakili Juma Nassoro, kuwa haikuwa sahihi kwa upande wa mashtaka kumfungulia kesi kwa shtaka la kukiuka amri ya mahakama, katika mahakama nyingine.
Badala yake Jaji Mkasimongwa amesema kuwa mjibu rufani huyo alipaswa kupelekwa katika mahakama ileile iliyomhukumu ajieleze ni kwa nini asifungwe kwa kukiuka amri yake, na kwamba kumfungulia shtaka hilo katika mahakama nyingine ni kinyume cha sheria.
Jaji Mkasimongwa amesema kuwa kama hakimu Moyo angezingatia hoja za mawakili wa utetezi basi shtaka hilo lingeishia palepale kwenye hatua ya hoja za kuwa au kutokuwa na kesi ya kujibu na isingefika kwenye hatua ya kuwa au kutokuwa na hatia.
Vilevile Jaji Mkasimongwa amesema kuwa kwa kusoma maelezo ya kosa la kuchochea watu kufanya mikusanyiko isiyo halali, hayatengenezi hilo kosa alilokuwa akidaiwa kwa kuwa katika mikutano yake alikuwa na kibali cha polisi, kama ambavyo polisi wenyewe walivyothibitisha mahakamani.
Jaji Mkasimongwa pia amesema kuwa kwa kusoma maelezo ya kosa la uchochezi na kuumiza imani za watu wengine, kwa hayatengenezi kosa hilo, kwa hakuna mahali popote ambapo imethibitishwa kuwa mtu fulani alichochewa kufanya mkusanyiko usio halali wala mtu aliyeumizwa imani yake.
Hii ni mara ya pili kwa Sheikh Ponda kuibwaga Serikali mahakamani katika rufaa, kwenye kesi za jinai ambazo amekuwa akifunguliwa.
Mara ya kwanza aliibwaga Serikali katika rufaa yake aliyoikata mwenyewe Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akipinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia hatiani kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la ardhi ya Chang’ombe Malkazi.
Katika kesi ya msingi ya jinai namba 245 ya mwaka 2012 Ponda na mwenzake Ponda na mwenzake Mukadamu Swaleh kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na shtaka la uchochezi.
Mashtaka mengine ambayo yalikuwa yakimkabili na wenzake 49 yalikuwa ni kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd.
Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mei 9, 2013, iliwaachia washtakiwa wote na ikamtia hatiani Ponda peke yake kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la ardhi ya Agritanza Ltd.
Hivyo ilimhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja ikimtaka asifanye kosa lingine lolote katika kipindi hicho, huku ikimtaka awe mlinda amani katika jamii.
Ponda kupitia kwa mawakili wake wakiongozwa na Nassoro alikata rufaa na Novemba 27, 2014 alishinda rufaa hiyo, baada ya Jaji Augustine Shangwa kukubaliana na rufaa yake na kumfutia hatia hiyo.
Akitoa hukumu hiyo Jaji Shangwa alikubaliana na hoja za Wakili Nassoro kuwa hapakwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo hilo.
Awali, Agosti 25, 2016, katika rufaa iliyotolewa uamuzi jana, Jaji Mkasimongwa aliamuru Sheikh Ponda atangazwe magazetini mahali popote pale alipo ili aweze kufika mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa dhidi yake.
Jaji Mkasimongwa alitoa amri hiyo kufuatia maombi ya upande wa mashtaka, baada ya Sheikh Ponda kutokutokea mahakamani hapo kwa mara ya pili kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa hiyo iliyokuwa ikimkabili.
Chanzo- Mwananchi
Social Plugin