SHIRIKA LA AGPAHI LAENDESHA ZOEZI LA UPIMAJI WA VVU KATIKA VITUO VYA AFYA JIJINI TANGA


Kushoto ni Muuguzi wa kituo cha Afya Ngamiani Lea Kakunya akichukua maelezo ya mkazi wa Jiji la Tanga ambaye alijitokeza kupima VVU wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani.
Wakazi wa Jiji la Tanga wakiingia kwenye viwanja vya Kituo cha Afya Ngamiani kwa ajili ya kupima VVU katika zoezi ambalo liliendeshwa na Shirika la AGPAHI katika vituo vya Afya vya Makorora,Ngamiani ,Pongwe na Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo ambapo zaidi ya wananchi 1900 walijtokeza kupima.
Kushoto ni Ochieng Makaranga ambaye ni Mratibu wa Huduma na Tiba kwa watu wenye VVU Kituo cha Afya Ngamiani Jijini Tanga akichukua maelezo ya mkazi wa Jiji hilo wakati wa zoezi la Upimaji wa VVU jana Disemba Mosi,2017. 
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Tanga wakiwa kwenye kituo cha Afya Makorora wakisubiri huduma ya kupima VVU.
Afisa Tabibu kutoka kituo cha Afya Makorora Jijini Tanga,Silvesta Leonard kulia akichukua maelezo kwa mmoja kati ya wananchi wa Jiji hilo ambaye alijitokeza kupima VVU Jana Disemba 1,2017
Muuguzi wa Afya katika Kituo cha Afya Makorora Jijini Tanga,Salima Athumani akimpima virusi vya Ukimwi
VVU mkazi wa Jiji hilo wakati wa upimaji huo uliokuwa ukiendeshwa na Shirika la AGPAHI
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Tanga waliojitokeza kupima VVU katika kituo cha Afya cha Makorora Jijini Tanga.

****
Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Care Initiative (AGPAHI) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga wameendesha zoezi la upimaji vya virusi vya Ukimwi kwa wakazi wa Jiji hilo huku zaidi ya wakazi 1900 wakijitokeza kupima na kupatiwa ushauri wa namna ya kuweza
kujikinga na maambukizi ya VVU .

Upimaji huo ulifanyika kwenye vituo vya Afya Makorora, Ngamiani, Pongwe na Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani inayoadhimishwa kila mwaka hapa
nchini. 

Zoezi hili la upimaji lililenga wanafamilia wa watu wanaoishi na
VVU katika jiji la Tanga. Upimaji huo ulianza siku ya Jumatano hadi Ijumaa (29 Novemba – 01 Disemba) ambayo ndiyo siku ya Ukimwi duniani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupima afya zao mkazi mmoja wa Donge Jijini Tanga, Zilipa Elangwe alisema zoezi hilo limekuwa ni zuri kwa sababu linasaidia watu kuweza kujua afya zao na namna ya kujikinga.

Alisema wanapokuwa wakijua afya zao inawasaidia kuweza kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kupelekea kuingia kwenye maambukizi ikiwemo kujiepusha na ngono zembe.

Aidha alisema huduma hiyo ya upimaji wa VVU ambayo imetolewa na Shirika la AGPAHI likishirikiana na halmashauri ya jiji la Tanga imewasaidia kujua afya zao kutokana na baadhi ya familia kutokuwa na uwezo wa kifedha kwenda kupima mara kwa mara hivyo ni jambo nzuri.

“Kwa kweli tunalishukuru sana Shirika la AGPAHI kwa kutuletea huduma hii ya upimaji wa VVU maana imetusaidia kujua afya zetu lakini pia kuchukua tahadhari ya kuhakikisha tunaepukana na maambukizi mapya",alisema.

Naye Saidi Sharifu mwenye miaka 72 aliliomba Shirika hilo kuendelea kutoa huduma za upimaji huo kila wakati ili kuweza kuwasaidia wananchi wanaokumbana na maambukizi waweze kujitambua na kuanza kutumia dawa.

Alisema ni ukweli usiopingika wapo watu wanaweza kukumbana na maambukizi kutokana na kushiriki tendo la ndoa bila kujijua hali zao hivyo kunapokuwa na huduma hiyo ya uhamasishaji upimaji wa VVU inasaidia kubaini hali yao ya kiafya na kuanza kuchukua hatua.

Naye Tabu Khamisi ambaye ni mkazi wa Makorora Jijini Tanga, alisisitiza kuwepo na uhamasishaji wa upimaji wa VVU wa mara kwa mara ili jamii iweze kupata fursa ya upimaji VVU na familia zao.

 Pia alisema upimaji huo umekuwa chachu ya wananchi kuweza kujitokeza kwa wingi kujua hali zao na namna nzuri ya kujikinga na maambukizi hususani wazazi waliojitokeza kwa wingi na watoto wao.

Naye Mratibu wa Ukimwi wa jiji la Tanga, Dr. Hamisi Mvugalo alisema juhudi ambazo zinafanywa na shirika la AGPAHI zinapaswa kuungwa mkono na kuwa endelevu kwani zina manufaa kwa jamii inayotuzunguka.

Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post