Shirikisho la Soka nchini (TFF), limeingia mkataba mnono na Kampuni ya Macron ambayo kuanzia sasa ndiyo mdhamini mkuu wa jezi za timu zote za Taifa; Taifa Stars, Twiga Stars na Serengeti Boys.
Aidha, udhamini huo wa miaka miwili wenye thamani ya Euro 700,000 zaidi ya Sh. bilioni 1.8 za Tanzania umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni jezi na vifaa vingine vya michezo, pamoja na fedha taslimu.
Akizungumza wakati wa utiaji rasmi saini ya makubaliano hayo wakati wa mkutano wa TFF na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau, alisema hiii ni mara ya kwanza kwa timu za Taifa kupata mkataba mnono kama huo.
"Kwa mwaka tutakuwa tukipata euro 150,000 ambapo kwa miaka miwili ni euro 300,000 (takriban Sh. milioni 800) hizo zikiwa ni mbali ya kupewa jezi na vifaa vingine, hii ni mara ya kwanza kwa timu zetu za taifa kupata udhamini wa jezi mkubwa kama huu," alisema Kidau.
Kwa upande wa Rais wa TFF, alisema bado wanaendelea kutafuta wadhamini kwa timu hiyo na ile ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ambayo haihusiki katika udhamini huo wa Macron.
"Mchakato huu umechukua muda mrefu na walikuwapo washindani wengi, lakini Kampuni ya Macron ndiyo imeshinda, na hatuishii hapo tu bado tunahitaji wadhamini wengine watakaoidhamini pia Kilimanjaro Stars.
"Kuna mengi tutakayofaidika katika mkataba huu, kwani pia tutakuwa tukipata sehemu ya mauzo ya jezi za timu ya Taifa na pia sasa itakuwa ni vigumu kutengenezwa na kuuzwa kiholela," alisema Karia.
Aliongeza kwa kufafanua kuwa awali ilikuwa vigumu kudhibiti watengenezaji na wauzaji holela kwa kuwa hata nembo ya TFF ilikuwa haijasajiliwa jambo ambalo kwa sasa limefanyika kabla ya kukamilisha mchakato huo wa udhamini.
Karia alisema faida ya uuzwaji wa jezi hiyo itaonekana kwa sasa kwa kuwa anaamini kutokana na Rais John Magufuli, kudhibiti uingizwaji uholela wa bidhaa nchini kwa kuimarisha ulinzi mipakani na bandarini, itakuwa ni vigumu kwa wale waliokuwa wakitumia ujanja huo kujinufaisha.
Social Plugin