Kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesimama.
Mwanasheria huyo wa Chadema, alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa ndani ya gari kwenye makazi yake mjini Dodoma Septemba 7,2017 na tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Picha iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii leo Jumanne Desemba 26,2017 inamuonyesha mbunge huyo akiwa amesimama kwa msaada wa madaktari wa mazoezi.
Baadaye Lissu ametuma ujumbe kwa MCL Digital akieleza kufurahia hatua hiyo.
Lissu katika mahojiano kadhaa aliyoyafanya na vyombo vya habari likiwemo gazeti la Mwananchi amekuwa akizungumza ama akiwa amelala au kukaa, lakini jana alisimama.
"Mungu ametupa zawadi na leo Lissu amesimama kwa mara ya kwanza kwa msaada wa physiotherapist, asante," amesema Hemed Ali, mmoja wa wasimamizi wa matibabu ya Lissu katika ujumbe wake.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) amesema, "Wiki iliyopita niliwataarifu kwamba madaktari wangu wamesema nitasimama, nitatembea na nitarudi Tanzania."
"Leo boxing day nimeweza kusimama kwa mguu mmoja kwa msaada wa mababu cheza kama inavyoonekana (katika picha aliyopigwa). Hatua inayofuata nitawajulisheni."
Na Elizabeth Edward na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Social Plugin