Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amemkaribisha Spika wa Bunge, Job Ndugai nchini Kenya kumjulia hali, akisema mwaka 2017 umekuwa wa kihistoria kwake na kwa Watanzania.
Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 katika makazi yake mjini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lissu alisema amesikia alichosema Spika Ndugai na kwamba, anachoweza kusema ni kuwa tangu alazwe Nairobi hakuna ujumbe wowote wa Bunge uliofika kumjulia hali.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Ndugai alisema vurugu za uchaguzi mkuu wa Kenya zilikuwa kikwazo kwake kwenda kumjulia hali Lissu na baada ya sikukuu atakwenda.
Alisema sintofahamu hiyo ilisababisha wanasiasa kwenda mahakamani hivyo kufanya uchaguzi mkuu kurudiwa na kuzua malumbano yaliyofanya kuwa na ‘Serikali kama ya mpito’.
Licha ya Spika Ndugai kutokwenda, kulikuwa na ujumbe wa wabunge wawili na mtumishi wa Bunge waliokwenda kumuona ambao hata hivyo, Lissu alirejea kauli aliyowahi kuitoa kwamba walikwenda kumuona wao binafsi.
Wabunge hao ni Mary Chatanda (Korogwe Mjini- CCM) na Fakharia Shomar Khamis (Viti Maalumu- CCM) pamoja na Kamishna wa Bunge ambaye jina lake halijawahi kutajwa.
“Hao anaowasema Spika walikuja, walikuja wao binafsi, kwani walipofika hapa niliwauliza kama wana ujumbe wa Spika wakakataa, nikamuuliza ofisa wa Bunge kama ana ujumbe wa Katibu wa Bunge akakataa, walikuja bila barua, waraka au hata kadi ya kunitakia pole,” alisema Lissu.
“Nilimweleza yule ofisa wa Bunge akamweleze kuwa Lissu ameuliza haki zake kwa mtu anayeumwa... mimi sihitaji fadhila, bali ni haki yangu kisheria.”
Akizungumza huku sauti yake ikionyesha ni mwenye afya njema, Lissu alisema sababu alizozitoa Spika Ndugai zingeweza kuwa na mashiko kama angezitoa kipindi alipokuwa akiumwa zaidi.
“Maelezo ya Spika yalikuwa ya kujitetea, angeweza kueleza wakati ule nikiwa na hali mbaya na mazingira ya Kenya yalivyokuwa angeeleweka lakini amesubiri hadi amebanwa, kelele zimepigwa na asingebanwa angeendelea kukaa kimya,” alisema Lissu
Kwa msisitizo Lissu alisema, “Kwa sababu amesema atakuja na mimi namsubiri aje na huo ujumbe atakaokuja nao, namsubiri sana sana... lengo langu na familia ni kuhakikisha haki inatendeka kama ilivyoandikwa katika sheria zetu.”
Kuhusu afya yake, Lissu alisema anaendelea vizuri na matibabu.
Alisema hataweza kusimama mapema kwa kuwa mguu wake ulivunjwa mara tatu na waliomshambulia, hivyo kupona kwake ni kwa taratibu.
Kuhusu ujumbe wake wa mwaka 2017, Lissu ambaye ni mwanasheria wa Chadema alisema, “Niwatakie kila la heri Watanzania wa ndani na nje ya nchi katika kipindi hiki cha sikukuu. Tunaufunga mwaka huku mamia ya wananchi wakiwa hawana makazi baada ya kubomolewa, uchumi wetu ukiwa haueleweki, tatizo la ajira, demokrasia inakandamizwa,” alisema.
Kwa sauti ya chini na yenye utulivu, Lissu alisema, “Sitachoka kuwashukuru Watanzania kwa maombi, michango yao, kunichangia damu na kuyafanya maisha yangu kuwa salama, nawashukuru sana sana.”
Pembeni mwa Lissu alikuwapo mkewe Alicia ambaye akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema, “Tunaendelea kuwashukuru Watanzania kwa yote waliyotufanyia. Tunawatakia maandalizi mema ya sikukuu.”
Alicia ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliongeza kuwa, “Ni matumaini yangu mwaka kesho utakuwa ni mzuri zaidi, mwaka mzuri kwetu kuliko tunaoumaliza wa giza nene.” Awali akitoa tathmini yake kwa mwaka 2017, Lissu alisema, “Ni mwaka wenye historia kubwa, umekuwa na matukio ambayo hayakuzoeleka, matukio ya utekaji ambayo wengine wanaonekana na wengine hawaonekani, matukio ya kushambuliwa. Yote haya tulikuwa tukiyasikia huko, sasa yamefika kwetu.”
“Tumeshuhudia chama kinachosema kinapendwa na wananchi kikilazimisha vyama vingine vichukiwe, umekuwa mwaka wa kihistoria, wenye matukio ya kipekee yasiyozoeleka, kwa kweli ni mwaka mgumu.”
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Social Plugin