Mbunge wa Singida Mashariki ambaye sasa Kenya akiendelea na matibabu kufuatia kupigwa risasi Septemba 7, 2017 amefunguka juu ya viongozi ambao wanasaliti CHADEMA na kusema jambo hilo lisiwatishe bali wao waendelee na kazi yao.
Tundu Lissu aliyasema hayo jana alipoonana Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Taifa, Patrick Ole Sosopi ambaye alimtembelea Mhe Lissu hospitali jijini Nairobi jana kumjulia hali
"Ndugu zangu Mhe Lissu ameweza kunieleza mambo mengi sana na binafsi naamini ameniagiza kwa niaba ya Baraza la Vijana na tutayetekeleza kwa maslahi mapana ya nchi na chama chetu, hajasita kuniambia kwamba hali ya siasa yetu ndani ya nchi yetu kwa biashara inayoendelea kununua Viongozi uchwara na wenye tamaa wa chama chetu, amesema tusipate hofu CHADEMA hatujaanza kusalitiwa leo na hao wanaondoka, sio ajabu hata kidogo kwani mbona Yesu aliwahi kusalitiwa tena na mwanafunzi wake na hakuacha kazi yake" aliandika Ole Sosopi
Aidha Sosopi aliendelea kusema kuwa Tundu Lissu amemweleza kuwa hata watu ambao waliwahi kuisaliti CHADEMA kipindi cha nyuma hawajapata mafanikio yoyote katika maisha yao
"Wanaotusaliti hawajawahi kuwa na mafanikio katika maisha yao, tusikate tamaa mapambano yaendelee. Mwisho kabisa Mhe. Lissu ametuma salamu nyingi kwa Watanzania wote wanaoendelea Kumchangia na Kumuombea, ameendelea kuwasihi waendelee kumchangia na kumuombea, maana Bunge na serikali wamekataa kabisa kumtibia ili hali kwa mujibu wa sheria ni haki yake" alisema Ole Sosopi