UTPC,MCT,TAMWA,THRDC,OJADACT WATOA TAMKO LA PAMOJA KUTOWEKA KWA MWANDISHI WA HABARI AZORY GWANDA

TAMKO LA PAMOJA LA WADAU WA USALAMA WA WANAHABARI KUHUSU KUTOWEKA KWA MWANDISHI WA HABARI WA KAMPUNI YA MWANANCHI COMMUNICATIONS LTD, NDUGU AZORY GWANDA


Utangulizi
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Waandishi Wanawake Tanzania (TAMWA; Umoja wa Waandishi wa Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (OJADACT), Umoja wa Vilabu vya Wanahabari Nchini( UTPC) pamoja na wadau wengine wa habari  tunapenda kulaani kwa pamoja kitendo cha kupelekwa kusikojulikana mwandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd,   Ndugu Azory Gwanda ambaye anaripotia huko Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani. Hadi sasa ni siku 18 zimepita tangu alipopotea mnamo tarehe 21 November 2017 bila kuwepo kwa jitihada za kutosha za kumtafuta  kutoka vyombo vya usalama. 

Baada ya kupata taarifa hizi Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari tuliunda kamati ndogo ya uchunguzi na kuituma huko Kibiti kuthibitsha taarifa hizi na kupata taarifa zaidi.

Kamati hiyo ilikwenda kufwatilia kinaga ubaga juu ya kupotea kwa ndugu Azory, mazingira ya kupotea kwake, sababu za kupotea, pamoja na jitihada zilizofanywa na polisi pamoja na Jamii inayomzunguka kuhakikisha anarudi.

 Timu hiyo ilipewa hadidu za rejea zifuatavyo; kuonana na mke wa ndugu Azory,  kupata historia yake, kuonana na ndugu jamaa na marafiki, majirani, serikali za mitaa, pamoja na Polisi.

Lengo la kuunda kamati hiyo ilikuwa ni kuepuka kufanyia kazi taarifa ambazo hatuna uhakika nazo. Taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa ndugu Azory alitoweka toka tarehe 21 Novemba 2017. 

Taarifa za kupotea kwake zimethibitishwa na mkewe  Bi Anna Penoni,  viongozi wa serikali za mtaa, ndugu na majirani. 

Historia fupi ya ndugu Azory na kazi zake za uandishi wa Habari

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati,  Ndugu Azory Gwanda ni Muha, mzaliwa wa Kigoma nchini Tanzania na ana umri wa miaka 42. 

Alipata elimu yake ya Msingi huko Kigoma katika shule ya Msingi Msimba kisha kuhamia shule ya Msingi Bulangamilwa iliyopo Tabora na baadae kujiunga na elimu ya Sekondari katika shule ya Sekondari Nanga iliyopo Igunga mkoani Tabora kisha kuhamia Dar es Salaam kwa kaka yake miaka ya 90.

 Tangu hapo ndugu Azory amesoma kozi mbali mbali fupi na ndefu ikiwa ni pamoja na kusomea Uandishi wa Habari na kupata Diploma katika Chuo cha Maarifa kilichopo jijini Dar es Salaam.

 Amekuwa mwandishi wa kujitegemea hadi pale alipojiunga na Kampuni ya Mwananchi ambapo pia anafanya kazi kama mwandishi binafsi anayeripotia gazeti la Mwananchi katika Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani. 

Kabla ya kujiunga na Kampuni ya Mwananchi ndugu Azory Gwanda alikuwa akifanya kazi katika kituo cha Redio cha WAPO FM kama mwandishi mwandamizi.

Kazi zake Wilayani  Kibiti-Mkoa wa Pwani

Itakumbukwa kwamba kati ya miaka ya  2016 na 2017, yalitokea machafuko na mauaji makubwa yaliyokuwa yakiratibiwa na watu wasiojulikana katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani ambapo ndugu Azory ndipo anapoishi na kufanya kazi za uandishi wa habari. 

Kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, kila mtu ana haki ya kupata na kutoa habari. 

Tafsiri ya Ibara hii haijamtenga Mwandishi wa Habari kwakuwa naye ni raia kama raia wengine wanaozungumziwa katika Katiba yetu hususani Ibara tajwa hapo juu. Hivyo kwa mazingira hayo usingetemea Mwandishi aache kazi yake ya kutoa habari kwani ana haki Kikatiba.

 Taarifa zinaonyesha ndugu Azori alikuwa mstari wa mbele katika kuandika  taarifa za mbalimbali za ukiukwaji wa haki, mauaji na matukio yanayotokana na hali ya Kibiti kiusalama.

Ndugu Azory Gwanda kama mwandishi amekuwa akitumia haki hiyo kuweza kutoa habari mbali mbali juu ya kile kilichokuwa kinatokea Wilayani Kibiti. 

Pia hata baada ya mapigano kupungua aliendelea kutafuta habari na kuufahamisha umma kwani zilisambaa habari kwamba bado kuna mauaji ya chini chini bado yanaendelea katika Wilaya hiyo, hivyo kwake bado alikuwa na jukumu la kufanya utafiti na kuweza kuuhabarisha umma wa Watanzania kupitia gazieti la Mwananchi. Ni kwa mazingira hayo ambayo tunadhani huenda yamepelekea usalama wake kuwa hatarini.

Shududa za Watu mbali mbali waliohojiwa kuhusiana na kupotea Azory Gwanda

(i) Mke wa ndugu Azory,
Mkewe Anna Penoni alibainisha kwamba mume wake alipotea siku ya jumanne tarehe 21 November 2017. Siku ya tukio, watu wapatao wanne walifika katika mji wa Kibiti wakiwa kwenye gari aina ya Land cruiser nyeupe. Walipofika katika eneo ambalo Ndugu Azori hupatikana muda mwingi, walimchukua na kwenda naye shambani kwa mkewe.

Walipofika shambani Ndugu Azori alimuuliza mkewe kutaka kujua ni sehemu gani ameweka funguo ya nyumba yao. 

Baada ya kupata maelezo kutoka kwa mke wake, waliondoka wakiwa kwenye gari hilo na kuelekea kusiko julikana huku akimpa maelezo mkewe kuwa amepata safari ya dharura na angeweza kurudi siku hiyo hiyo au siku inayofuata.

 Tangu siku hiyo Ndugu Azori hajaonekana hadi sasa. Bi Anna Penoni pia aliripoti kwamba baada ya tukio hilo, alikagua vitu vyote vilivyokuwamo ndani na kukuta baadhi ya nyaraka kama vile vyeti na vitambulisho vikiwa havionekani.

Mke wa Ndugu Azori ameshafikisha taarifa za kutokea kwa tukio hilo katika kituo cha Jeshi la Polisi Kibiti tangu tarehe 23/11/2017. Faili lenye namba Kibiti/RB/1496/2017 lilifunguliwa na Polisi waliahidi kufanya uchunguzi.

 Ni jambo la kusikitisha kwamba hadi sasa bado Polisi hawajatoa taarifa yoyote kuhusu jitihada walizofanya kuweza kufanikisha kupatikana kwa ndugu Azory. Aidha Bi Anna ameomba vyombo husika kusaidia kupatikana kwa mume wake kwani ndio tegemeo lake na hana msaada mwingine. 

Akiongea kwa masikitiko makubwa, Bi Anna alisema; “kwa sasa mimi ni mjamzito na siku yoyote nitajifungua, mume wangu ndiye msaada mkubwa kwangu, naomba serikali isikie kilio changu mume wangu aweze kurudi akiwa salama”.

(ii) Majirani wa ndugu Azory
Baadhi ya majirani waliohojiwa wamedai kwamba, siku ya tukio waliliona gari aina Land Cruiser likiingia nyumbani kwa ndugu Azory ila walidhani kuwa huenda ni wafanyakazi wenzake ndugu Azory kwakuwa si mara ya kwanza magari kuingia nyumbani kwake.

 Walisema kwamba, gari hilo halikuonesha dalili zozote kwamba watu waliokuwamo ni majambazi bali alihisi labda ni waandisihi wenzake au watu wa Serikali. Alidai kuwa gari hiyo ilikaa muda wa dakika 15 nyumbani kwa ndugu Azory kabla ya kuelekea kusikojulikana.

(iii) Marafiki zake

Baadhi ya marafiki zake waliohojiwa walisema kwamba, huenda Azory amekamatwa kutokana na kazi yake ya uandishi na wanaamini waliomchukua ni watu ambao mwisho wa siku watamrudisha kwakuwa hata wakati wanamchukua hakukuwa na viashiria vyovyote kuwa watu hao walikuwa na nia ya kumfanyia ubaya wowote. 

 Wapo wanaoamini huenda amechukuliwa kuhojiwa na vyombo vya usalama na baada ya muda watamwachia.

(iv) Ushuhuda wa Serikali za mitaa
Kwa upande wa viongozi wa serikali za mtaa anaoishi ndugu Azory, hawakuwa na taarifa zozote mpaka pale mke wa ndugu Azory alipowapa taarifa juu ya tukio hilo. 

Hata hivyo viongozi wa mtaa walisema hawana wasi wasi na mwandishi huyo kwani amekuwa akipigania haki za watu wengi kwa muda mrefu na hivyo isingekuwa rahisi kwa mwandishi huyo kutekwa na watu wasiojulikana.  Na wao pia wanaamini huenda yupo kwenye mikono salama na anaweza akaachiwa muda wowote.

(v) Ushuhuda wa Polisi Mkoa wa Pwani:
Timu ya ufuatiliaji  ilipata wasaa wa kuongea na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ambaye alikiri kupokea taarifa kwamba tukio la kupotea kwa ndugu Azory Gwanda ni kweli liliripotiwa katika kituo cha polisi Kibiti na kupewa RB No.Kibiti/RB/1496/2017. 

Hata hivyo kamanda huyo wa polisi alikaririwa akisema, kwakuwa ndugu Azory Gwanda alimuaga mke wake kwamba anaenda safarini na atarudi huenda ni kweli atarudi. 

Aliendelea kusema kwamba kwakuwa suala hilo tayari limesharipotiwa polisi wao wanandelea kulifanyia kazi na endapo watapata taarifa zitakazoweza kusaidia kupatikana kwa ndugu Azory, wataufahamisha umma na mke wake kwakuwa alishaacha mawasiliano yake katika kituo hicho cha polisi. Aliongeza pia kusema kwamba ni mapema kusema ni nani aliyemteka kwakuwa bado uchunguzi wa polisi unaendelea.

Usalama wa Raia na Mali zao Kisheria

Ni lazima ikumbukwe kwamba kila mtu anayo haki ya ulinzi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Vyombo vya dola vina wajibu wa kuwalinda raia na mali zao. Ibara ya 7 ya Azimio juu ya Ulinzi wa Watu wote dhidi ya Upotevu inasema kwamba hali yoyote ile, iwe tishio la vita, hali ya vita, migogoro ya kisiasa ndani au nyingine ya dharura ya umma, haiwezi kuhalalisha kupotea kwa mtu.

Pia katika sehemu ya 2, Kifungu cha 5 (1) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi kinasema; "Jeshi la Polisi litaajiriwa katika Jamhuri yote ya Muungano kwa ajili ya kulinda amani, kudumisha sheria na utulivu, kuzuia na kugundua uhalifu, kuwakamata na kuwaongoza watuhumiwa na kulinda mali, na katika utekelezaji wa majukumu yote hayo watakuwa na haki ya kubeba silaha." Hii yote ni mamlaka waliyopewa polisi katika kuwalinda raia na mali zao.

Tumesikitishwa na ongozeko la watu kutoweka na kwenda pasipojulikana na hakuna chochote kinachofanyika au kuonekana kufanya kuzuia suala hili linalozidi kuota mizizi katika jamii. Makundi ya watetezi, waandishi, wanasiasa na wasanii wamesharepotiwa kupotea na kutoweka. Kati yao wapo waliokotwa wameumizwa vibaya, wapo ambao hadi leo hawajulikana walipo na wengine kurudi wakiwa na hofu kubwa.  

Watetezi wengi wa haki na wanahabari wamekuwa wakipata matatizo haya kwa kiasi kikubwa na kutokana na mara nyingi chanagamoto wanazokumbana nazo ni kwasababu ya kazi zao. Hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha kwamba Ndugu Azori anapatikana.  Mikataba ya Kimataifa na Kikanda inakataa aina yoyote ile ya utekaji na kupotezwa kwa nguvu. 

Katika mazingira haya tunayoshughudia kwa sasa ni dhahiri kwamba hali ya watetezi wa haki za binadamu si salama tena. 

Tuliliomba jeshi la polisi kutupa ulinzi ili kuweza kuandamana kwa amani hadi ofisi za IGP ili tupeleke hoja zetu na kilio chetu kiweze kusikilizwa lakini tumesikitishwa na majibu ya Msemaji wa Jeshi la Polisi kwa niaba ya IGP kukataa maandamano hayo ya amani yasifanyike.

 Aidha, tunashukuru uongozi kwakuwa wameturuhusu kuunda timu ya watu wawakilishi wachache kwenda kuonana na IGP ili aweze kusikiliza hoja zetu. Tunaamini tutapata ushirikiano mkubwa na suluhu ya matatizo yanayowakabili watetezi wa haki za binadamu kwa sasa.

Kutokana na uchunguzi huu mdogo ni matumaini yetu kuwa Azory hadi  sasa yupo hai na huenda ameshikiliwa kwa malengo yasiyojulikana na watu wasiojuilikana.  Kurudi  kwake  kutategemea ni jinsi gani kilio cha wadau na familia yake vitazingatiwa na wahusika.  

Wito Wetu:

I. Vyombo vya ulinzi na usalama Tanzania vihakikishe kuwa kila raia anaishi kwa uhuru na usalama nchini Tanzania. Jeshi la Polisi liwe tayari kuwalinda raia na mali zao dhidi ya jambo lolote baya.

II. AZAKI, vyombo vya habari na umma wa watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinalenga au kuashiria kuzuia uhuru wa maoni nchini Tanzania.Tunapaswa sote kukemea kwa sauti moja hali yoyote inayozuia kufurahia haki zetu. Leo ni Azori na wengine haijulikani siku wala saa ya kutekwa au kupotea kwa mwandishi , mtetezi au raia wa kawaida.

III. Watetezi wa haki za binadamu tuungane na kupaza sauti zetu kwa pamoja juu ya hali hii ya watu kutoweka inayozidi kushika kasi chini

IV. Kutokan na wimbi hili la utekaji na kutoweka kwa Watanzania wenzetu, Serikali ya Tanzania inapaswa kutia sahihi na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa kwa Ajili ya Ulinzi wa Watu Wote Waliotekwa na Kuwekwa Vizuini pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Utesaji na Vitendo Vingine vya Kikatili vinavyotweza utu wa Binadamu.

V. Serikali ihakikishe wahusika wote wa tukio la kupotea kwa Mwandishi Azory Gwanda wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sehria ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na kukomesha matukio kama haya siku za usoni.

VI. Viongozi wa siasa na Bunge waone haja ya kulijadili suala hili la utekajji na kupotea kwa watanzania wenzetu na kuja na maazimio.

VII. Mashirika na Asasi za Kimataifa waweze kuungana na Watanzania kupinga uonevu na uminywaji wa haki ya uhuru wa habari nchini Tanzania.

VIII. Tunaviomba vyombo vya habari viendelee kufanya uchunguzi na kuhabarisha umma juu ya kupotea kwa ndugu Azory Gwanda.

IX. Watanzania wote tushirikine kuwafichuwa hawa wote wenye nia ya kuwaangamiza watanzania wenzao bila hatia yoyote.

X. Kipekee tunapenda kuipongeza Mwananchi Communications Limited kwa kuchukulia tatizo hili kwa umakini na kuonyesha kuguswa na tunaviomba vyombo vya habari vyote viwe na moyo huu pale waandishi wao wanapopata matatizo bila kujali hadhi yao au aina ya mikataba waliyo nayo.


Issued on 09Th December, 2017
Signed on behalf of
And:
Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC)
Media Council of Tanzania (MCT)
Union of Tanzania Press Clubs (UTPC)
The Organization of Journalist against Drug Abuse and Crime in Tanzania (OJADACT)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post