Idadi ya watumishi wanaorudisha fomu za tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaongezeka kwa kadri muda unavyosonga.
Baadhi ya watumishi hao wametuma wawakilishi kuzirejesha baada ya kuzijaza.
Waandishi wa MCL Digital walioweka kambi katika ofisi za Sekretarieti hiyo Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Desemba 29,2017 wameshuhudia baadhi ya watumishi wa umma wakipishana kurudisha na kujaza fomu kazi ambayo inapaswa kukamilika Desemba 31,2017.
Kamishana wa Sekretarieti hiyo, Jaji Harold Nsekela amesema sheria imeitaja Desemba 31 kuwa ni siku ya mwisho ya kupokea fomu hizo na kwamba leo ilipaswa kuwa mwisho wa kuzipokea kwa kuwa Jumamosi na Jumapili si siku za kazi.
Kwa kutambua changamoto hiyo, amesema kesho Jumamosi Desemba 30,2017 watafanya kazi.
"Kesho ni siku ya mapumziko lakini tumeona tufungue ofisi ili kuwapa fursa watumishi kurejesha fomu," amesema.
Jaji Nsekela amewaasa watumishi wa umma kujiwekea utaratibu wa kuzirudisha fomu hizo mapema.
"Haya mambo ya kusubiri mwisho mwisho yanaweza kuleta shida, si lazima usubiri hadi Desemba 31," amesema.
Kuhusu viongozi waliotuma wawakilishi kurudisha fomu amesema hakuna tatizo ila inapotokea zina makosa hasara inakuwa kwa mhusika.
Miongoni mwa waliotuma wawakilishi ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni aliyemwagiza katibu wake kuzirejesha baada ya kuzijaza.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alirejesha fomu yake mwenyewe.
Sophia akiwa ameambatana na mwanaye wa kiume, amesema anamshukuru Mungu kwa kumaliza mchakato huo.
“Nimejaza vizuri na kurejesha na kama ukikosea unaelekezwa. Nimeshawasilisha kila kitu kinachohitajika. Natoa wito kwa wale wasiorejesha wafanye hima wasisubiri dakika ya mwisho," amesema.
Wengine waliorejesha fomu lakini hawakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari ni mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa na aliyekuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah.
Na Bakari Kiango na Elizabeth Edward, Mwananchi
Social Plugin