Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI WATANO WATUPWA JELA KWA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA SIMIYU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoani Simiyu iwamehukumu kwenda jela kwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu au kulipa faini ya shilingi milioni 1.5 maafisa watano, baada ya kukutwa na hatia ya kutumia madaraka yao vibaya.

Maafisa hao walikuwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani mkoani hapa, ambao ni Ramadhani Zongo (Afisa maendeleo ya jamii-amestaafu), Stephen Mayani (Afisa Ugavi), Maduhu Magili (Mhandisi wa maji) Joackim Leba (Afisa Utumishi), na Leonard Batigashaga (Afisa Biashara).


Hukumu hiyo imetolewa juzi na Hakimu mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Simiyu John Nkwabi, ambapo maafisa hao walikuwa wajumbe wa bodi ya zabuni ya halmashauri.


Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu, Polycarp Mtega aliambia mahakama kuwa washitakiwa wanakabiliwa na kesi ya Jinai namba 30 ya 2016 chini ya kifungu cha 31 cha sheria ya makosa ya rushwa namba 11 ya mwaka 2007.


Mtega alieleza kuwa washtakiwa wote wanatuhumiwa kwa kosa la kubadilisha maamuzi ya timu ya tadhimini ya kumpata mkadarasi wa ujenzi wa bwawa katika halmashauri hiyo kinyume na kifungu cha 75 cha sheria ya manunuzi namba 07 ya mwaka 2011.


Alisema kuwa maafisa hao kwa kujua kuwa wako kinyume cha sheria walitumia madaraka yao vibaya, kubadilisha mkandarasi aliyepitishwa na timu hiyo katika ujenzi wa bwawa la umwagiliaji lililoko katika kijiji cha Ikungulyambeshi kwa shilingi Bilioni 1.8.


Alisema tarehe 07/05/2012 maafisa hao wakiwa chini ya Mwenyekiti wa bodi ya zabuni ya halmashauri, Makamu mwenyekiti, pamoja na wajumbe walimbadilisha Mkandarasi GAT Engineering Co.Ltd aliyepitishwa na timu ya tathimini na badala yake kumpatia Jossam & Company Ltd kinyume na utaratibu.


Aliongeza kuwa Mkandarasi aliyepitishwa na maafisa hao kampuni yake ilikuwa na uwezo wa daraja tano (v), wakati tangazo la zabuni lilihitaji mkandarasi mwenye darasa la nne hadi moja (1V-1) ambaye GAT Engineering Co.Ltd alistahili.


Baada ya maelezo hayo Mwendesha mashtaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili kuwa fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuacha kutumia madaraka yao vibaya.


Kwa upande wao washtakiwa hao waliiomba Mahakama hiyo kuwapunguzia kifungo kutokana na kosa hilo kuwa la kwanza, huku wengine wakidai kuwa wana umri mkubwa na wategemewa na familia zao.


Mara baada ya utetezi huo washtakiwa wote walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu kila mmoja kwenda jela au kulipa faini shilingi Milioni 1.5 ambapo walikosa faini hiyo na kupelekwa gerezani.
Na Costantine Mathias - Simiyu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com