Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ASHANGAA MTAMBO WA KUTENGENEZA MBEGU ZA PAMBA KUJENGWA MBEYA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza mtambo wa kutengenezea mbegu za pamba ulioko mkoani Mbeya, kuondolewa mara moja na kupelekwa kwenye mikoa inayolima zao hilo huku akihoji sababu za msingi zilizochangia mtambo huo kuwekwa huko.


Akizungumza na wadau wa zao hilo Waziri Mkuu alitoa agizo hilo na kuitaka wizara inayohusika kuchukua hatua mara moja huku akivitaka viwanda vya ndani vyenye uwezo wa kuzalisha mbegu kujitokeza.


Amesema haiwezekani mtambo unaotengeneza mbegu za pamba ukawekwa kwenye mkoa ambao haulimi zao hilo na kuhoji kulikuwa na sababu gani ya msingi ya kuwekwa mkoani Mbeya, ndipo aliamua kuagiza kuondolewa na kupelekwa kwenye mikoa inayolima pamba.


Hata hivyo Majaliwa alisema kiwanda cha Quiton ambacho kimewekeza nchini kwa ajili ya kutengeneza mbegu za pamba aina ya Quiton lakini cha kusikitisha mpaka msimu wa kilimo unafika hakuna mbegu na hii kampuni inamilikiwa na Wazimbabwe na wao wanalima pamba nchini kwao katika hili tutafakari.


‘’Tunataka zao la pamba liwe na mafanikio makubwa na haya yote yanapaswa kusimamiwa na watumishi wa serikali ili kuweza kumkomboa mkulima wa pamba, kulima kilimo chenye tija ambacho kitawaletea mabadiliko ya kiuchumi kwani asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo” amesema waziri mkuu.


Kwa upande wake Waziri wa Chakula na Ushirika Dk Charles Tizeba amesema katika msimu uliopita jumla ya kilo 133 milioni za pamba zimezalishwa , ambapo kwenye msimu wa mwaka huu wanatarajia kuzalisha kilo 600 milioni za pamba huku uzalishaji wa tija utaongezeka kwa ekari kutoka kilo 200 hadi 500.


Amesema ekari 1,100,000 zimepandwa mbegu zisizo na manyoya ambapo lengo ni kufikia ekari 3,000,000 milioni na kuongeza kuwa umetumika utaalamu katika upandaji ,huku akibainisha kuwa tayari kuna chupa 4,764,000 za dawa za kuuwa wadudu zimepatikana ambazo zitasambazwa kwa wakulima kwa awamu nne.


Awali akizungumza kwenye mkutano huo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amesema jumla ya ekari 128,668 za pamba zimelimwa mpaka sasa mkoani Shinyanga, kutoka kwa wakulima 24,175 ambapo wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com