Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amekataa kutoa usajili kwa Shule ya Msingi Njalu iliyopo wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu kutokana na kutokidhi vigezo.
Shule hiyo imejengwa na wananchi kwa kushirikiana na mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Silanga.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika jana katika shule hiyo iliyopewa jina la Njalu kutokana na mchango wa mbunge huyo katika ujenzi, Profesa Ndalichako alisema shule hiyo haijakidhi vigezo vya usajili.
Mbele ya wakazi wa Kijiji cha Habiya ilipo shule hiyo, waziri Ndalichako alikataa ombi la mbunge huyo kuisajili na kuagiza upungufu uliopo urekebishwe kwanza kabla ya wizara kuisajili shule hiyo ya umma.
Miongoni mwa upungufu huo ni kuwa na vyumba vitano pekee vya madarasa badala ya vinane vinavyohitajika.
Mengine ni matundu ya vyoo, ambayo kati ya 10 yanayohitajika, yapo matano pekee, huku ikiwa na chumba kimoja cha ofisi ya walimu.
Profesa Ndalichako alisema wizara itatoa mifuko 100 ya saruji kusaidia kuondoa upungufu uliopo.
“Tumeona kuna upungufu hatutaweza kutoa kibali cha kuisajili, badala yake mkamilishe yanayohitajika kwa utaratibu wa kisheria wa kufungua shule. Niwahakikishie kuwa, Wizara ya Elimu hatuna urasimu ni lazima tuwe makini kwa kusimamia vigezo hivyo,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema licha ya kuwapo kwa mahitaji ya shule katika eneo hilo ambalo lina wanafunzi wapatao 633, ni lazima kuzingatia vigezo ambavyo vitakaguliwa na wataalamu kutoka idara ya udhibiti ubora wa elimu na ofisi ya ofisa elimu wilaya.
Awali, Silanga alielekeza lawama kwa watumishi wa Serikali na hasa wa idara ya elimu mkoani Simiyu kwa kushindwa kutumia utaalamu wao kuwaelimisha wananchi kuhusu vigezo vinavyotakiwa kabla ya shule kusajiliwa.
“Timu ya wataalamu ishuke itoe maelekezo. Majengo mengi yanavunjwa, wasimamizi tunao lakini hawatekelezi majukumu yao hivyo watimize wajibu wao kuliko kuwakatisha tamaa wananchi katika kuchangia shughuli za maendeleo,” alisema.
Silanga alimwomba Waziri Ndalichako kuwapatia usajili wakati wakiendelea kushughulikia upungufu uliojitokeza kwa kipindi cha muda mfupi kabla ya shule kufunguliwa Januari 8 mwakani ombi ambalo hata hivyo, lilikataliwa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema hawawezi kuwaadhibu wananchi na mbunge, hivyo ni lazima wahakikishe upungufu uliopo unaondolewa kabla ya Januari 15 mwakani.
Katika kuunga mkono jitihada hizo, Mtaka alitoa mifuko 50 ya saruji; huku mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Chilangi pia akitoa mifuko 50.
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imeahidi kutoa mabati na mbao zitakazohitajika katika ujenzi.
Social Plugin