Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BABA AUA MTOTO WAKE KWA KUMPIGA NGUMI NA MATEKE AKIDAI SIYO WAKE




Mtoto aitwaye Benedicto Salumu(13) mkazi wa kitongoji cha Saint Maria kata ya Matai wilayani Kalambo mkoani Rukwa ameuawa kwa kupigwa ngumi na mateke tumboni na baba yake akidai siyo mtoto wake ni wa mwanaume mwingine.

Tukio hilo limetokea Januari 1,2018 majira ya saa 4 usiku ambapo Pius Salum(46) alimpiga mtoto huyo baada ya ugomvi kuzuka baina yake na mkewe Hilda Mpangamila (37).

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kitongoji hicho Rafael Sinyangwe alisema kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na ugomvi baina ya baba wa mtoto aitwaye Pius Salum(46) na mkewe Hilda Mpangamila (37) akimtuhumu kuwa mtoto huyo si wa kwake. 

"Mara kadhaa amekuwa akiwalalamikia ndugu zake kuwa mkewe alibeba ujauzito wa mtoto huyo wakati akiwa amekwenda kutafuta maisha na aliporudi alihisi kama mkewe ni mjamzito",alieleza mwenyekiti. 

"Katika kipindi chote alichokuwa akimlea mtoto huyo alikuwa hana mapenzi naye kama watoto wake wengine akiamini kuwa siyo mtoto wake na mara kwa mara alikuwa akigombana na mkewe akidai analea mtoto ambaye si wake",aliongeza Mwenyekiti huyo. 

Aliiambia Malunde1 blog kuwa siku ya tukio hilo mtuhumiwa akiwa ametoka kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya 2018 huku akiwa amelewa aliingia chumbani na kukuta mtoto huyo akiwa amelala na kisha kuanza kumpiga na ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo tumboni hadi kupeleka kifo chake. 

Aliongeza kuwa baada ya kumuua alimpiga pia mke wake akidai kuwa amemsababishia kulea mtoto asiyekuwa wake kwa muda mrefu hali ambayo ilikuwa ikimuudhi na kumkosesha amani . 

Na Walter Mguluchuma- Malunde1 blog Rukwa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com