Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wanachama wa CCM kuwa kimepokea taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa kutakuwa na uchaguzi wa marudio katika Kata na Majimbo yaliyotajwa hapo juu.
Wanachama wote wenye sifa za msingi kwa mujibu wa Katiba ya Nchi na waliokidhi vigezo vya uanachama kwa mujibu wa Katiba ya CCM na Kanuni zake wanahamasishwa kujitokeza ili kuomba ridhaa ya Chama kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi huu wa marudio isipokuwa na kama inakavyoelekezwa na taarifa hii.
Aidha Chama kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu na kisayansi, na zilizosheheni siasa za hoja na zinazojikita katika kushughulika na shida za wananchi na hatimaye kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huu wa marudio. Kwa maana hii, msisitizo unawekwa kwa wanao omba ridhaa ya kugombea, vikao vya uchujaji na mapendekezo, na vikao vya uteuzi kuzingatia Misingi ya Maadili na kuhakikisha waombaji wana akisi uaminifu, uadilifu, uchapakazi, heshima kwa watu, ukubalifu wa imani, siasa na itikadi ya CCM, nidhamu kwa chama na wawe watu ambao umma wa wananchi unawatambua kwa nafasi yao katika jamii inapokuja katika kushughulika na shida zao.
KWA WAOMBA DHAMANA YA UDIWANI
Wana CCM ambao wamejipima na kujitafakari na kuona wanatosha, wanakumbushwa kwamba kuchukua fomu ya ugombea udiwani katika Ofisi za Kata tajwa hapo juu ni tarehe 8-11 Januari 2018. Mwisho wa kurudisha fomu ni tarehe 11 Januari 2018 saa 10:00 jioni. Gharama ya fomu ni Shilingi 10,000/- tu za Kitanzania.
Wajumbe wa Mikutano Mikuu ya Kata watapiga kura za maoni tarehe 12 Januari 2018. Kamati za Siasa za Kata zitajadili na kutoa mapendekezo kwa Kamati za Siasa za Wilaya tarehe 13 Januari 2018.
Kamati za Siasa za Wilaya zitajadili na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Mkoa tarehe 14 Januari 2018. Kamati za Siasa za Mikoa zitajadili na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu za Mikoa tarehe 16 Januari 2018. Halmashauri Kuu za Mikoa zitajadili na kufanya uteuzi wa mwisho tarehe 17 Januari 2018
Wagombea walioteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushiriki katika uchaguzi wa Udiwani katika Kata nne watachukua fomu kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata katika kata husika tarehe 18-19 Januari 2018 na zoezi hili litafanyika chini ya usimamizi wa Katibu wa CCM wa Wilaya.
UCHAGUZI WA MARUDIO KWA MAJIMBO YA SIHA NA KINONDONI
Baada ya tafakuri na tathimini ya kina, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwa mamlaka iliyokasimiwa kwake na Kikao cha Halmshauri Kuu ya Taifa (NEC) imemteua Ndg. Dkt. Godwin Mollel kusimama na kugombea Jimbo la Siha, Mkoa wa Kilimanjaro na Ndg. Maulid Mtulia kusimama na kugombea Jimbo la Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha wagombea wa Ubunge wanaelekezwa kufika katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mikoa husika na kupokea maelekezo yahusuyo Uchaguzi kutoka kwa Makatibu wa CCM wa Mikoa hiyo siku ya Jumanne, tarehe 9 Januari 2018 bila kukosa.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na,
HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
06 Januari 2018