DC RUANGWA ATOA WIKI MBILI KWA MKANDARASI PART INTERPLAN LIMITED


Mkuu wa wilaya Ruangwa mkoani L indi Joseph Joseph Mkririkiti amempa wiki mbili mkandarasi anayesimamia ujenzi wa jengo la ofisi za mkuu wa wilaya hiyo Part Interplan Limited kuhakikisha anakamilisha mara moja ujenzi wa jengo hilo la sivyo hatua za kisheria kuchukuliwa kutokana na uzembe anaoundeleza wa kutokukamilisha kwa ujenzi huo bila sababu za msingi.


Akizungumza baada ya kutembelea jengo hilo Januari  20,2018 kuona maendeleo ya ujenzi na kuonekana hakuna shughuli zinazoendelea za kuelekea kumaliziwa kwa jengo hilo, mkuu wa wilaya hiyo amesema jengo husika lilianza mchakato wake mwaka 2008 kwa kampuni iliyofahamika kwa jina la Ruvuma Construction na baadaye kubadilishwa jina ikawa inaitwa Part Interplan Limited.

“Ndani ya wiki mbili asiporipoti mimi nitaomba tuvunje naye mkataba ili tupate mtu mwingine ambaye atatumalizia hii kazi” alisema Mkirikiti.


Aidha amesema wamefanya jitihada nyingi sana za kumtafuta mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha kazi hiyo na kwamba makadirio ya awali wakati wanaanza ujenzi huo ilikadiriwa shilingi  milioni 321 mpaka kukamilika lakini kadri walivyokuwa wanachelewa kukamilisha kazi kwa miaka yote zaidi ya kumi gharama zinaendelea kupanda na kuwa juu sana.

“Jitihada zetu ilikuwa walau akamilishe walau ofisi ya mkuu wa wilaya ili aweze kuhamia lakini nayo imeshindikana”, alisema Mkirikiti.

Pia ameeleza kuwa alimuomba katibu tawala wa mkoa wa Lindi ili kuhakikisha mkandarasi huyo awe analipwa pesa site ambako ujenzi unaendelea afanye kazi na kulipwa papo hapo badala ya kumlipa kwa kumwekea kiasi chote kama mzabuni wakati eneo la kazi hajafika jambo ambalo ameeleeza ndiyo limesaidia mpaka kufikia hapo lilipofikia jengo kwa sasa.

“Huyu mkandarasi ifike mahali kama yafaa sheria ichukue mkondo wake kwa sababu ni mkandarasi ambaye kwa kweli anaonyesha uvivu sana katika kukamilisha kazi yake” ,amesema mkuu huyo wa wilaya.

Wilaya ya Ruangwa ni miongoni mwa zile za wilaya 6 zinazounda mkoa wa Lindi ambapo ukiacha, Kilwa, Lindi manispaa, Lindi vijijini, Liwale na Nachingwea, wilaya hii ilikuja kuwa mpya kutokana na sehemu kubwa iliyokuwa ya Lindi vijijini kuonekana kuwa na eneo pana ambalo lilitosha kuanzishwa wilaya yake na ndipo mwaka 1992 wilaya hii ilianzishwa.

Wilaya hiyo mpya ikajikuta ikikosa miundombinu ya kutosha kwa ofisi zote za utawala na kulazimika baadhi ya ofisi kuwepo katika majengo ya kujishikiza wakati utaratibu wa kujengwa kwa ofisi husika ukiendelea.

Ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo inayotumiwa kwa sasa ni ile ya Majengo ya zamani chakavu ambayo kwa mujibu wa uhitaji ofisi zinazotakiwa kuwepo katika jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya eneo hilo hazitoshi na baadhi ya ofisi kulazimika kuwepo katika chumba kimoja zaidi ya ofisi mbili jambo ambalo si sahihi kwani kila ofisi ina taratibu na miko yake ya kazi.

Kutokana na kukamilika kwa jengo hilo jipya kungeweza kutoa nafasi za kukamilika kila ofisi inayostahili kuwepo katika jengo la mkuu wa wilaya ikiwa ni pamoja na ofisi za vizazi na vifo, jeshi la akiba, zimamoto, uhamiaji, na ofisi zingine zinazostahili kuwa hapo ili kuwahudumia wananchi katika mazingira ambayo yanakuwa ni bora zaidi.


Mkuu wa wilaya ya Ruangwa Joseph Joseph Mkirikiti
Jengo linalotelekezwa na mkandarasi Part Interplan Limited ambalo ndiyo ofisi mpya ya mkuu wa wilaya ya Ruangwa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post