Siku moja baada ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza kumtaka msanii Gift Stanford ‘Gigy Money’, kuripoti ofisini kwake, msanii huyo ameamua kwenda Baraza la Sanaa Tanzania( Basata).
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Gigy ambaye alijipatia umaarufu kutokana na kupiga picha za kutatanisha na kuzirusha katika mitandao mbalimbali ya kijamii, amesema ameamua kwenda Basata baada ya kuambiwa waziri hayupo.
Hata hivyo, amesema mpaka sasa hajui kosa analoitiwa na kama ni picha za utupu mbona ameshaacha tabia hiyo siku nyingi na sasa yupo busy kulea mimba yake.
“Najua wapo watu wanaodhani naitwa kwa ajili ya tabia zangu za kupiga picha za utupu, lakini mimi hayo mambo nishayaacha muda mrefu nadhani kwa wanaonijua Gigy wa sasa hivi sio wa kipindi kile, ila ngoja nisubiri waziri atakachoniambia japo najiona sina kosa lolote nililotenda kwa sasa tangu Rais alipotoa onyo kwa wasanii wanaovaa vibaya.
“Pia kwa wale wanaodhani labda ni kutokana na wimbo wangu wa Papa, binafsi sina wasiwasi nayo kwa kuwa mimi nilimaanisha samaki, sasa kama kuna watu wameitafsiri kivingine ni wao,” amesema .
Kwa upande wake Katibu wa Basata, Godfrey Mngereza alikiri msanii huyo kufika katika ofisi zao zilizopo Ilala leo na kueleza kwamba hilo halimuondolei kuitikia wito wa waziri kwa kuwa yeye ndiye aliyemuita.
Mngereza amesema alichokiona kwa msanii huyo ni kwenda kwao akijua kwamba baraza hilo ndio mlezi wa wasanii na kubainisha kuwa hata wao walikuwa hawafurahishwi na aliyokuwa anayafanya msanii huyo japo hawajawahi kumuita hata siku moja.
Na Nasra Abdallah, Mwananchi
Social Plugin