Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo amepokewa kwa nderemo na wafuasi wa chama hicho.
Lowassa ambaye kwa mara ya kwanza leo Jumamosi Januari 27,2018 amevaa gwanda tangu ajiunge na Chadema mwaka 2015 aliwasili ofisi za chama hicho kanda ya Pwani zilizoko Magomeni, ambako yalianza maandamano kuelekea Mwananyamala ulikofanyika mkutano wa hadhara wa kampeni.
Mkutano huo umefanyika katika uwanja wa Ali Mapilau, Mwananyamala.
Akiongea katika mkutano huo, Lowassa amefunguka na kuwataka wanachama na viongozi wa CHADEMA kuacha kumtaja taja mgombea Ubunge wa CCM Kinondoni Maulid Mtulia kwani mtu huyo ni wa hovyo hastaili kutajwa tajwa kwani kufanya hivyo ni kumpa kichwa.
"Kwanza nawashauri huyu Mtulia msimseme seme sana wanini huyu, mtu hovyo kabisa huyu mnampa kichwa tu sasa mtu hovyo hapaswi kuchukua muda wenu kumjadili bali nachotaka tushughulike kuwaelimisha wananchi wa Kinondoni kwanini wanastahili kutupa sisi kura, habari ya huyu bwana tuachane naye, hawa CCM hawaeleweki kule Moshi na Korogwe tulishinda lakini wakaja kusema tumeshindwa hivyo nataka kusema saizi tujiandae kulinda kura zetu" alisema Lowassa
Mbali na hilo Lowassa alimnadi Salum Mwalimu kwa kusema kuwa ni kijana safi ambaye anastahili kwenda Bungeni kuwasemea wananchi wa Kinondoni
Akizungumzia hatua ya Lowassa kuvaa Gwanda, Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Kinondoni, Rose Moshi amesema anadhihirisha kuwa ni kamanda na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi naye.
"Tulikuwa na hofu alipokwenda Ikulu, kuvaa kwake gwanda kunaonyesha kuwa ni mwenzetu," amesema.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Jerome Ulomi amesema Lowassa amedhihirisha kuwa ni mwana Chadema.