Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amemwambia Rais John Magufuli kuwa CCM ni chama chake, japo kwa sasa amekiacha licha ya kushiriki kukijenga na kwamba hawezi kwenda kinyume nacho.
Kingunge aliyetangaza kuhama chama hicho tawala Oktoba 4, 2015 alitoa kauli hiyo jana akiwa kitandani Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiuguza majeraha ya kung’atwa na mbwa takriban siku tano zilizopita nyumbani kwake.
Jana, Rais Magufuli alikwenda kumtembelea mwanasiasa huyo na wakati wakipeana mkono, alitumia nafasi hiyo kueleza jinsi alivyoijenga CCM, ambayo ni miongoni mwa vyama vichache vya ukombozi vinavyoongoza Serikali barani Afrika.
Wakati akiuguza majeraha hospitalini hapo, Kingunge alifiwa na mkewe, Peras huku mwanaye Kinje Ngombale akieleza jinsi walivyopata wakati mgumu kumueleza jambo hilo kwa kuwa kifo hicho kilitokea wakati mwanasiasa huyo mkongwe akiwa usingizini baada ya kutoka chumba cha upasuaji.
Huku akionekana kutulia katika picha za video zilizotolewa na Ikulu, Kingunge alisema, “CCM ni chama changu, nimetoka tu nimeacha, lakini nimefanya kazi zote, nimekijenga mimi kile chama. Hakiwezi kuwa kinyume changu hata kidogo.”
Rais Magufuli alimshukuru kwa kukiri kwake huko na kusema, “Ahsante sana. Hayo maneno yako ni muhimu sana, kwamba CCM ni chama chako hakiwezi kuwa kinyume chako. Kwa hiyo siku zote wewe ni CCM ndani ya moyo wako. Mungu akubariki sana.”
Taarifa iliyotolewa baadaye na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kwamba mbali ya Rais Magufuli kumtembelea Mzee Kingunge katika wodi ya Mwaisela, pia aliwajulia hali baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wakiwamo pacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti.
Akiwa katika wodi ya Mwaisela, Dk Ibrahim Mkoma wa hospitali hiyo alimweleza Rais Magufuli kuwa hali ya Mzee Kingunge inaendelea vizuri huku mkongwe huyo wa siasa akimshukuru Rais kwa kwenda kumuona na kumweleza kuwa sasa anajisikia nafuu baada ya kupata matibabu.
Pamoja na kumpa pole na kumuombea apone haraka, Rais Magufuli alisema anatambua mchango mkubwa wa Mzee Kingunge katika siasa na maendeleo ya nchi.
Pia alikwenda katika wodi ya Sewahaji na kuwajulia hali Richard Kajumulo ambaye ni kaka wa mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka, Said Abeid Salim, Amina Ismail Shirwa, Mzee Hamad Lila na alimpa pole Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Dk Zainab Chaula aliyefiwa na mama yake mzazi wakati Rais akiwa wodini humo.
Akiwa JKCI, Maria na Consolata walimshukuru Rais Magufuli kwa kwenda kuwaona na kuwapa pole na walitumia fursa hiyo kuongoza sala ya kumuombea Rais na nchi. Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema matibabu ya wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (Rucu) yanakwenda vizuri huku akibainisha kwamba taasisi hiyo imetoa matibabu kwa wagonjwa wa moyo 14,000 katika mwaka uliopita na inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa utoaji wa huduma bora za matibabu ya moyo.
Rais Magufuli aliwashukuru na kuwapongeza madaktari wa hospitali hizo kwa kazi kubwa wanayofanya kutibu wagonjwa akiahidi kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha huduma zaidi.
Wachambuzi wanena
Walipotakiwa kutoa maoni yao juu ya kauli hiyo ya Mzee Kingunge, baadhi ya wachambuzi wa siasa walisema inawezekana ni kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Magufuli ndani ya CCM tangu alipoingia madarakani.
Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema kumekuwa na mabadiliko makubwa ndani ya CCM yanayowavutia waliondoka kurejea.
“Kingunge ni mwanasiasa anayejua kuchagua maneno. Alikwenda Ukawa kwa sababu ya kumuunga mkono kijana wake aliyekuwa akimpenda, Edward Lowassa. Siyo kwamba alipenda sera za Ukawa wala za Mbowe (Freeman-Mwenyekiti Chadema),” alisema Profesa Bana.
“Lakini sasa hali inaonyesha tofauti, mambo anayosimamia Rais Magufuli yanafanya mtu aweze kujitambulisha kama mwana CCM.”
Hata hivyo, alisema ni mapema mno kusema moja kwa moja kwamba kuna mabadiliko ya kweli ndani ya chama hicho.
“Chama mbadala cha Chadema ndiyo kinaonekana kinadidimia. Kwa maoni yangu ili chama hicho kirudi, ni lazima asilimia 80 ya viongozi wake akiwamo mwenyekiti na katibu wajiuzulu, ikiwezekana wawarudishe hata kina Zitto (Kabwe),” alisema Profesa Bana.
Lakini mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani, Njelu Kasaka alitofautiana na Profesa Bana akisema kauli ya Kingunge haihusiani na mabadiliko ya CCM kwa kuwa bado hayaonekani.
“Kwa sababu kujiunga au kujitoa kwenye chama ni uamuzi wa mtu binafsi, suala la nani kafanya nini ni lazima ueleze. Hata mimi niliwahi kusema chama kilikuwa kimetoka nje ya mstari ila sasa kinarudi, lakini wasiwasi wangu itachukua muda mrefu mno kukirudisha. Kwa hiyo huo ni uamuzi binafsi wa Kingunge,” alisema Kasaka.
Kingunge alipoiacha CCM
Oktoba 4, 2015 Kingunge akizungumza na vyombo vya habari nyumbani kwake Mwananyamala, Dar es Salaam alisema ameachana na CCM kwa kuwa imeishiwa pumzi.
Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama hicho kufanyika huku jina la Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa likikatwa na Rais Magufuli akapitishwa.
“Kuongoza nchi ni kama kupanda mlima, utafika mahala pumzi zinakwisha na huwezi kuendelea mbele na ukijaribu kwenda mbele unabaki palepale, na hivi ndivyo CCM, kimeishiwa pumzi na kimebaki palepale hakiwezi tena kupanda mlima,” alisema.
Akiuzungumzia mchakato wa kupata mgombea urais, Kingunge alirejea historia ya CCM mwaka 1995 akisema utaratibu ulikuwa ni Kamati Kuu ya chama hicho kuwaita wanachama wote walioomba kugombea urais ili kuwasikiliza na kuwahoji.
“Nimeshiriki kwa muda mrefu kuhakikisha kuwa ndani ya CCM kuna demokrasia ambayo kwa sasa inapigwa teke. Katiba kazi yake ni kutuunganisha wote, hivyo hatuna budi kuiheshimu, lakini viongozi wetu sasa wamekuwa wabinafsi na wanafanya mambo wanavyotaka wenyewe na sijui wanafanya kwa masilahi ya nani,” alisema Kingunge.
“Mwaka 2005, utaratibu huu pia ulitumika. Mgombea mmoja hakuridhika na maamuzi ya Kamati kuu kukata jina lake. Alikata rufaa Halmashauri Kuu ya chama ambako pia alisikilizwa. Ingawa hakushinda rufaa yake, lakini demokrasia ya kuwasikiliza watu iliheshimiwa tofauti na sasa watu wanafanyiwa vitendo vya udhalilishaji.”
Hata hivyo Kingunge aliyejiunga na TANU mwaka 1954 akiwa na kadi nambari 7, hakujiunga na chama kingine cha siasa, bali alisema anaunga mkono upande wa mabadiliko.
Na Elias Msuya, Mwananchi
Social Plugin