Mahasimu wakubwa katika mchakato wa kuwania urais ndani ya CCM mwaka 2015, Edward Lowassa na Bernard Membe jana walikutana jijini Dar es Salaam na kuzungumza kwa zaidi ya saa tatu.
Wawili hao, waliotajwa kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa wakati huo ndani ya chama hicho tawala, walikutana katika msiba wa mama wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima eneo la Salasala jijini hapa.
Kukutana kwa Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu, na Membe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne na kuzungumza kwa muda mrefu, kumeibua kumbukumbu ya upinzani waliokuwa nao katika mchakato huo uliowaondoa wote na kuzuia majina yao kufika kwenye Mkutano Mkuu wa CCM.
Rais John Magufuli aliibuka kidedea kati ya makada watatu waliopelekwa kupigiwa kura na Mkutano Mkuu, baada ya kuvuka Halmashauri Kuu, ambayo ilionyesha kuchukizwa na jina la Lowassa kutopitishwa na Kamati Kuu kwa kuimba wimbo na kumtaja kwa jina mbunge huyo wa zamani wa Monduli.
Wakati huo makundi ya watia nia hao yalichuana vikali mpaka kufikia hatua ya kuibua hali ya sintofahamu katika mikutano na vikao vya kuchambua majina ya makada 38 waliojitokeza ndani ya chama hicho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Jana, wawili hao walikaa pamoja na kuzungumza kwa zaidi ya saa tatu huku kila mmoja akionekana kumsikiliza mwenzake kwa makini.
Membe, aliyekuwa amevaa shati jeupe la mikono mirefu na suruali nyeusi, ndiye aliyeonekana kuwa mzungumzaji zaidi huku Lowassa aliyekuwa amevaa kaunda suti nyeusi, akiwa msikilizaji zaidi.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo aliiambia Mwananchi kuwa mara baada ya kukutana, wawili hao walizungumza kwa zaidi ya saa tatu.
“Kwa kweli wamezungumza mengi sana. Sijui walichokuwa wakizungumza, lakini walikutana msibani saa 5:00 asubuhi na mpaka sasa (saa 8:30 mchana) bado wapo,” alisema Liongo alipotafutwa na gazeti hili muda huo.
Katika maongezi hayo, Membe alionekana kumuinamia zaidi Lowassa huku akitumia ishara ya mikono katika kueleza licha ya kuwa walikuwa wakizungumza taratibu, kwa umakini na kutabasamu mara kadhaa.
Kuna wakati mazungumzo yao yalikuwa yanakatishwa na watu waliowafuata ili kuwasalimu, lakini waliendelea kuzungumza hadi walipoamua kuondoka. Walisimama pamoja na kuondoka eneo hilo na baadaye kuongea kwa kipindi kifupi kabla ya kila mmoja kupanda kwenye gari lake.
Kabla ya kuanza mchakato wa kuchukua fomu za urais CCM, wafuasi wao waliingia kwenye malumbano makali na wote wawili walikuwa kwenye kundi la makada sita waliozuiwa kujihusisha na shughuli zozote kwa mwaka mmoja baada ya chama hicho kuona kuwa walikiuka taratibu.
Baada ya kuchukua fomu na kuzunguka kutafuta wadhamini, Kamati Kuu ya CCM ilikuwa na jukumu la kuchuja majina ya makada 38 hadi kubakia majina yasiyozidi matano ambayo yalipelekwa Halmashauri Kuu (NEC)kwa ajili ya kupigiwa kura na kubakiza matatu. Majina matatu yaliyopitishwa katika kikao cha NEC yalipigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Julai 11 na 12, 2015 na jina la Dk Magufuli kuibuka kidedea.
Baadhi ya mambo yaliyotajwa kuzingatiwa katika kufanya uteuzi ni kutafuta mtu atakayeondoa makundi, suala la Muungano, jinsia, eneo la kijiografia na rekodi ya mtia nia na kukubalika kwa kada hasa katika kipindi hicho ambacho upinzani ulikuwa umeimarika.
Julai 10, 2015 Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa manane ilikata jina la Lowassa, baadaye chama hicho kiliwataja waliopitishwa kuwa ni Membe, Dk Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali.
Dakika chache baada ya kikao hicho kumalizika, wajumbe watatu wa Kamati Kuu, akiwamo aliyekuwa mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi waliongea na waandishi wa habari kueleza kutokubaliana na jinsi mchujo ulivyofanyika, wakidai kuwa si majina yote yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
Dk Nchimbi, ambaye alikuwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba, walisema kikao hicho hakikufuata kanuni na hayakuhusisha mgombea anayekubalika, ingawa hawakumtaja.
CHANZO- MWANANCHI